NA KHAMISUU ABDALLAH

ALIYESHINDWA kutii sheria za usalama barabarani apandishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mshitakiwa huyo ni Abdulmalik Jussa Ameir (23) mkaazi wa Bweleo wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo akiwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Nassem Faki Mfaume na kusomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Rajab Mussa.

Kwa mujibu wa hati yamashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo ilidai kwamba, Septemba 9, mwaka huu majira ya saa 3:55 asubuhi huko Fumba Polisi akiwa anaendesha Vespa yenye namba Z 704 GW, akitokea Fumba Ziwani kuelekea Fumba Bondeni, alipatikana akiendesha Vespa hiyo akiwa hakuvaa kofia ngumu (helment), kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Hati hiyo ilidai kwamba kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 130 (1) (4) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.  

Mshitakiwa huyo baada ya kusomewa shitaka hilo alikubali na kuiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa madai kwamba hilo kosa lake la kwanza, huku upande wa mashitaka ukidai kwamba hauna kumbukumbu ya makosa ya nyuma kwa mshitakiwa huyo.

Hakimu wa mahakama hiyo baada ya kusikiliza maelezo ya pande mbili alimtaka mshitakiwa huyo kulipafaini ya shilingi 30,000 na akishindwa akatumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi miwili.

Mshitakiwa huyo alilipa fedha hizo ilikujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo.