NA TIMA SALEHE,DAR ES SALAAM

VINARA wa Ligi Kuu Bara, klabu ya Azam FC jana  Oktoba 26 wamekutana na kisiki cha mpingo, baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza ndani ya ligi kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Azam FC ilikuwa imecheza jumla ya mechi saba bila kupoteza na ilifunga mabao 14 huku ikifungwa mabao mawili pekee, na kipa wao namba moja David Kissu alikuwa ameokoa mipira ya hatari golini mwake mara  sita kati ya mechi saba.

Jana ameshuhudia nyavu zake zikitikiswa na Jaffary Kibaya dakika ya 62 na kufanya ufalme wake wa kuokoa mipira kuyeyuka huku timu hiyo inayonolewa na kocha Mkuu, Aristica Cioaba ikiyeyusha pointi tatu kwa mara ya kwanza msimu wa 2020/21.

Mbali na mchezo huo mchezo mwengine uliwakutanisha mabingwa watetezi Simba dhidi ya Ruvu Shooting, mchezo ambao ulimalizika kwa Simba kupoteza mechi ya pili mfulululizo baada ya kufungwa bao 1-0, mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Simba ilitoka kupoteza mchezo wiki iliyopita baada ya kufungwa bao 1-0 na Prison huko Rukwa, ambapo jana iliendelea kupoteza tena.

Boa pekee la Ruvu lilipachikwa wavuni na mchezaji Full Maganga katika dakika ya 35.