NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa Azam FC umesema  mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar halikuwa fungu lao la kupata ndio maana wamepoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Azam FC inayofundishwa na kocha mkuu, Aristica Cioaba ilikuwa imecheza jumla ya mechi saba bila kupoteza, ilipoteza mchezo wake wa kwanza juzi Oktoba 26, Uwanja wa Jamhuri Morogoro kwa kufungwa na Mtibwa Sugar.

Bao pekee la ushindi lililowapoteza Azam FC lilipachikwa na Jaffay Kibaya dakika ya 62 na kudumu mpaka dakika ya 90 kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema wachezaji wamefanya kazi nzuri mwisho wa siku matokeo hayakuwa upande wetu.

“Bado ni sehemu ya mchezo na tutaendelea kupambana kwani haikuwa fungu letu la kushinda tunajipanga kwa ajili ya mechi zijazo, tuna kikosi kizuri na wachezaji wapo vizuri.”

Kwenye mchezo wa juzi nyota wawili wa kikosi cha kwanza walikosekana ambao ni Obrey Chirwa ambaye ni mshambuliaji mwenye mabao manne alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.

Salum Abubakar, Sure Boy alikuwa ana adhabu ya kadi tatu za njano, yeye ana pasi moja ya bao.

Azam FC ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 21 baada ya kucheza mechi nane, Mtibwa Sugar ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 11 nayo imecheza mechi nane.