BAKU,AZERBAIJAN

ARMENIA na Azerbaijan zimetuhumiana kwa kukiuka mpango wa kiutu wa kusitisha mapigano katika mkoa wa Nagorno-Karabakh muda mfupi baada ya kuanza kutekelezwa .

Wizara ya ulinzi ya Azerbaijan mjini Baku ilisema kuwa wanajeshi wake walishambuliwa kwa risasi katika kijiji kimoja,madai ambayo yalipingwa na maofisa wa Armenia walioko jimbo la Nagorno-Karabakh.

Jamhuri hizo mbili za uliokuwa muungano wa Kisovieti zimekuwa katika mapigano kuhusiana na jimbo hilo linalogombaniwa, ambalo kwa miongo mingi limedhibitiwa na wanajeshi wa Kikristo wa Armenia lakini linazingatiwa na Umoja wa Mataifa kuwa sehemu ya Azerbaijan iliyo na Waislamu wengi.

Msemaji wa jeshi la Armenia Shushan Stepanyan alisema kuwa mashambulizi yaliongezeka mpakani mwa mkoa huo.