Mkoani Queens yaanza kujinoa tena

HABIBA ZARALI, PEMBA

“KATIKA sekta ya michezo kwa upande wetu sisi wanawake ugonjwa wa corona umeturejesha nyuma kiasi kikubwa kimaendeleo”.

Licha ya kuweka miili yetu sawa lakini michezo kwetu ni ajira ambayo tunaitegemea katika maisha yetu haswa lakini kuja kwa corona imetufanya tusuwesuwe.

Hayo ni maneno ya Ramla Juma Khamis ambae ni mwenyekiti wa mpira wa miguu Wilaya ya Mkoani wakati alipokuwa akizungumza na makala hii kuhusiana na ugonjwa wa corona ulivyoathiri wanamichezo wanawake.

Ramla ambae pia ni mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya Mkoani Queens anasema kipindi cha mripuko wa ugonjwa wa corona walitakiwa wachezaji kubaki nyumbani kwa ajili ya kuepuka maambukizi lakini wao liliwarejesha nyuma kimichezo.

Anasema ili uwe mchezaji mzuri basi uhakikishe unafanya mazoezi ya kutosha lkn kwa kipindi hicho wao walishindwa kuendelea nalo hilo.

“Kukaa kwetu pamoja na kufanya mazoezi tunaibuwa chanagamoto nyingi ambazo zinatukwaza na hatimae tunazirekebisha na kuendelea mbele’alisema.

Anaendelea kusema kuwa katika kipindi chote cha kukaa ndani kwa kutizama hatma ya maradhi ya corona walikosa kucheza ligi mbalimbali ambazo hizo ndio zinazowaingizia kipato.

Anazitaja njia ambazo zinawaingizia kipato ikiwemo michango na hata wafadhili wa timu na ligi husika lakini sasa yote yamepotea.

“Nyungu ni moto wa mwanzo sasaivi hata kama tukirejea haitokuwa kama awali mpaka tuchukuwe muda kidogo kurejesha kama zamani kweli corona imetuathiri katika michezo”alisema kwa unyonge.

WACHEZAJI WANASEMAJE

Rukia Omar Ali mchezaji wa Mkoani Queens anasema kabla ya Corona alikuwa anaendelea vizuri  kutokana na agizo la kutokusanyika alilazimika kuacha mazoezi.

Mpira bila kutoka kucheza mechi za kirafiki na kufanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya ligi kuu huwezi kuleta mafanikio jambo ambalo limetukumba wakati huu wa corona.

Anasema ingawa serikali imeruhusu mikusanyiko lakini bado michezo haijachanganya vyema kwani hata mashabiki wao hawako kawaida.

“Tulikuwa tukifanya mazoezi kundi zima la wanawake ambao tuliwashajihisha lakini kuja kwa corona wengi bado hawajarudi uwanjani hadi sasa”, alisema.

Hamida Juma amani mchezaji wa Mkoani Queens anasema hata kipato chake kimerudi chini  kwani kipindi cha kukaa ndani kwa corona ndicho kilichokuwa cha msimu wa uchezaji.

Anasema kutoka muda huo hadi sasa hali ya kimichezo inadorora jambo ambalo linarejesha nyuma hali za maisha kwa  wachezaji.

Mwanafedha Juma mchezaji wa Mkoani Queens anasema waliweza kushajihisha akina mama wengi wenye matatizo ya sukari na presha huku na wao wakijiweka sawa na program zao lakini sasa wengi hawajarudi uwanjani .

Anasema kufika katika mazoezi kwa wanawake hao waliweza kupunguza matatizo kwa asilimia kubwa jambo ambalo lilikuwa ni faida kwa wanawake.

MKUFUNZI WA TIMU YA WANAWAKE ANASEMAJE

Abubakar Mzee Mohamed anasema baada ya kuanza maradhi ya corona mwezi Machi mwaka huu Serikali iliweka mikakati mbali mbali ikiwemo kuzuwia mikusanyiko katika maeneo yote hata kwenye viwanja vya michezo.

Anasema baada yamikakati hiyo ndipo wakalazimika kufunga mazoezi na kughairisha ratiba zote za michuwano ya kirafiki.

Anasema ni pengo kubwa lililojitokeza lakini hakukuwa na jinsi kwani maradhi ya corona ni janga la dunia nzima.

“Najuwa kama mtikisiko kwa wanamichezo wetu hawa wanawake kwani kama kawaida ya akina mama walivo mpaka wapembejewe kwenye baadhi ya mambo sasa wakiwa tayari kumeingia unyovu wa kujikalia nyumbani lazima kurudi itakuwa na uzito ila tunapambana”alisema na matani kidogo.

VIONGOZI WANASEMAJE

Msaidizi katibu ZFF mkoa wa Kusini Pemba Nassour Hakim Haji anasema katika kipindi cha Corona kipato cha wachezaji kilikuwa chini kutokana na kuwa hakukuwa na uchezaji wa ligi zozote.

Anasema kusimama kwa ligi kuliwawezesha wachezaji kurudi nyuma maendeleo yao na baadhi ya ligi ziliweza kusambaratika.

Anasema kwa upande wa taifa pia limeweza kupata hasara kwa kukosekana kwa sekta ya michezo kwani michango imekuwa haipo pamoja na kutoweka kwa wafadhili kwani hata nao pia janga la corona kuwakumba.

“Kwa upande wa wananchi nao janga la corona limewakosesha kuona burudani na kukata tamaa badala yake wakajishughulisha na pirika nyengine”alisema.

Anasema hata ligi kwa mwaka huu zimechelewa na kalenda ya mashindano imesogea mbele ila anasema watahakikisha viporo vilivobakia vinamalizwa.

Katibu wa ZFF wilaya ya Mkoani Juma Said Mohamed anasema licha ya corona kuathiri sekta ya michezo lakini bado wanamichezo wanatakiwa kupambana kwa hali zote ili kurejesha hali ya kawaida.

Alisema ni vyema kurudi uwanjani na kuweza kufanya mazoezi kwa bidii ili kuweza kupambana vyema katika ligi.

Katibu alivitaka vilabu vyote vinavyoendeleza mechi za mbuzi , Ng’ombe , kuku cup na nyengine kuhakikisha wanafika katika ofisi za ZFF wilaya ili kupata usajili ambao mwisho wa siku ndio msimamizi wao litokeapo tatizo kwao.

“Lengo ni kuleta matokeo mazuri katika michezo sasa kujitajidi kupambana na kurejesha hadhi kwa wanamichezo ni jambo la busara”alisema.

MASHABIKI WANASEMAJE

Fatma Kombo juma anasema kuzorota kwa timu za wanawake hakuoneshi sura nzuri ni vyema wakaendelea kwa kasi ili waweze kushinda ligi zinazokuja.

Anasema kushinda kwa wanawake katika mechi mbalimbali kunazidisha hamasa kwa wapenzi wa michezo.

Hadia Rashid Abdalla anasema ili kuhakikisha wanapata ushindi bado wanawake wanahitaji mazoezi ya nguvu ya pumzi na wepesi kwa ajili ya kurejesha viwango vyao kama walivyokuwa hapo awali.

Anasema kukaa na kujisahau kufanya mazoezi ni hatari  kutaweza kuzigharimu timu zetu za wanawake ambazo tunajivunia uwepo wake.

Haji Massoud Hilal anasema iwapo wanawake wataamuwa kurudi uwanjani na kufanya mazoezi vizuri na kwa bidii katika michezo wanauwezo wa kuwashinda hata akina baba.

Anasema wanawake wanauwezo mkubwa wa kustahamili dhiki mwilini kuliko wanaume jambo ambalo linatia moyo katika mambo mengi wanayoyafanya.

Akitowa ushauri Asha Bakar Mohamed (52) anasema ni vyema timu yetu ya wanawake kurudi uwanjani kama zamani kwani kutofanya hivyo kunaweza kurejesha nyuma maendeleo yao katika michezo.

Sekta ya michezo hususan mpira wa miguu kwa upande wa wanawake ni moja kati ya sekta zenye uwezo mkubwa wa kuitangaza nchi kimichezo ngazi ya kitaifa na kimataifa na kupata umaarufu mkubwa.

Katika sekta hiyo pia serikali inapata kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi wake hususan vijana ambao ndio kundi kubwa hapa nchini pia hupelekea kuibua na kukuza vipaji mbalimbali.

Hivyo sababu hizo na nyengine nying imepelekea busara za Raisi wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein kuanzisha uibuwaji wa vipaji ngazi za chini ikiwemo mashuleni kwa kupitia  sports 55.