Ni ilani yenye kutekelezeka, inayowajali wananchi wa makundi yote

NA MWANDISHI WETU, PEMBA

TAKRIBAN wiki mbili zijazo taifa la Tanzania litaingia katika uchaguzi mkuu wa kuwachagua viongozi watakaoongoza nchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kwa mujibu wa ilani ya tume ya uchaguzi ni kwamba uchaguzi ni mkataba baina ya wanao omba kupigiwa kura na wananchi (viongozi) na watakao piga kura ni wananchi.

Kwa maana hiyo wananchi ambao watapiga kura wanahitaji kuyasikia yale yaliomo kwenye Ilani za Uchaguzi na sio yale yalio nje ya Ilani ambayo mengi hayatekelezeki.

Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-25, inakurasa 303 inayoeleza mambo mbali mbali ambayo inawaahidi kuwatekelezea wananchi ambao ndio wapiga kura mara baada ya kuwapa ridhaa ya kuendelea tena kuongoza ndani ya nchi hii.

Lakufurahisha ni kuona katika ukurasa 187 mpaka ukurasa 296, inaeleza mambo maalumu ambayo Viongozi wa chama cha Mapinduzi (CCM) wakipewa ridhaa na wananchi itayatekeleza kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote na katika nyanja tafauti tafauti za kijamii.

Kama ni hivyo basi tujiulize katika Ilani za vyama 17 ambavyo vimesimamisha wagombea Urais Zanzibar, jee zimeweka mambo maalumu ambayo yanaeleza lipi watawafanyia wananchi pale vitakapopewa ridhaa na wananchi kuongoza dola kama vile ilivyo ya Chama cha Mapinduzi ?.

Dk, Hussein Ali Mwinyi, mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) anapozungumzia suala la ukuzaji wa Uchumi limo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho.

Ibara ya 139 inasema CCM itaendeleza kasi ya mageuzi ya uchumi na kuwa wa kisasa na utakaowanufaisha wananchi waliowengi hasa Vijana.

Ilani hiyo kifungu (b) katika suala la hali ya uchumi inaeleza CCM itatengeneza fursa moya za ajira rasmi na sekta zisizo rasmi 300,000 ifikapo mwaka 2025 hususan kwa vijana ili kusaidia kupunguza umaskini.

Aidha kifungu (c) (ii) inasema CCM itaimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka wastani wa shilingi bilion 800.0 kwa mwaka 2019 hadi shilingi trillion 1.55 mwaka 2025.

Dk, Hussein Ali Mwinyi mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati akiinadi ilani ya chama hicho kwa wananchi katika sekta ya Utalii husema CCM itatekeleza mipango madhubuti katika sekta hiyo kukuza Utalii.

Kwa mfano kifungu cha 153 cha Ilani hiyo kinaeleza Utalii ni sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar katika kuchangia pato la Taifa, fedha za kigeni na kutowa fursa nyingi za ajira kwa kutambuwa kuwa Zanzibar inavivutio vingi vya kipekee vya utalii.

Inasema kuwa mkazo mkubwa utawekwa katika ushirikishwaji wa jamii, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuongeza idadi ya watalii wa daraja la juu na watakaokaa kwa muda mrefu .

Katika Ilani hiyo CCM itaielekeza SMZ kufanya yafuatayo;-kifungu (a) (i) itahakikisha kunakuwa na ongezeka kwa idadi ya Wageni kutoka 538,264 mwaka 2019 hadi kufikia 850,000 mwaka 2025.

Kifungu cha (a) (ii) cha ilani hiyo kuhusiana na utalii , kutaongezeka kwa siku za ukaazi kutoka wasatani wa siku saba mwaka 2019 hadi kufikia siku nane mwaka 2025.

Na kifungu (a) (iii) kinasema kutaongezeka kwa matumizi ya mgeni kutoka wastani wa Dola za Kimarekani 262 kwa siku mwaka 2019 hadi kufikia Dola za Kimarekani 350 mwaka 2025.

Kwa mnasaba huo Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi, anayoyaeleza katika mikutano yake ya Kampeni iwe ya hadhara ama ya makundi maalumu ni yale yaliomo kwenye Ilani na haendi nje ya matakwa ya Ilani hiyo.

Hapa tunapata utafauti kati ya Mgombea wa Chama cha Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi na baadhi ya wagombea wenzake wa vyama vya upinzani kutoka katika vyama vyengine vya Siasa kwani wanayoyaeleza kwa wapiga kura hayaendani na yale walioyaandika kwenye ilani zao.

Kwa mtu ambae amewahi kuzisoma Ilani za vyama mbali mbali ataona kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM kweli amedhamiria kutekeleza maendeleo ya kweli na sio kuwadanganya  wapiga kura  kama wanavyofanya baadhi ya wagombea.

Mmoja wa Mwananchi aliezungumza na makala haya aliejitambulisha kwa jina la Ali, alisema baada ya kuziangalia ilani mbali mbali za vyama vikuu vya Siasa ni ya chama cha Mapinduzi pekee ndio ilani yake inayotekelezeka ukilinganisha na ilani za vyama vyengine.

Alieleza mgombea yoyote anaeleza mambo yalio nje ya Ilani ya chama chake anawadanganya wapiga kura kwani mengi anayoyaahidi hayatekelezeki.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar

“Mimi sio mwanasiasa lakini nimekuwa nikisoma baadhi ya Ilani kupitia kwenye mtandao pale ninapopata nafasi lakini nimeona Mgombea wa CCM Dk. Hussein Mwinyi, anayoyanadi ni yale  ambayo yameandikwa kwenye Ilani ya  chama chake na haendi nje ya hapo,” alisema.

“Ukiniuliza ni nani naweza kumpa kura kwa sasa katika ya wagombea 17 wa Urais kwa sasa nitakudanganya kwani ni mapema mno kutowa uamuzi ila Ilani ya CCM inakwenda na wakati na yaliomo yanatekelezeka kwa vile mengi yalishaanzwa kufanywa kitambo,” alieleza.

Nae Kijana Mohammed Ali Salim, alisema kimtazamo Mgombea wa CCM anakubalika kwa makundi yote ibakie ushabiki wa vyama na Ilani ya chama chake anapoinadi inatia matumaini haiko kinyume na lile liliandikwa.

Alifahamisha baadhi ya wagombea wamekuwa hawaelezi yale yaliomo kwenye Ilani zao na kwamba huiga yale ya ilani ya CCM.

“Mfano kuna mgombea amesikika akisema akichaguliwa atazungumza na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kukubaliana upya mambo ya muungano hilo sio jambo  rahisi kufanyika”, alisema.

Alisema wanalohitaji wapiga kura nikuelezwa yaliomo katika kitabu cha Ilani kwani ndio yaliokubaliwa na Chama husika na sio kupewa maneno yanayotoka mdomoni mwa mtu binafsi.

Akizungumzia kuhusiana na kipindi hichi cha Mikutano ya Kampeni ni tofauti  na miaka iliopita kwa kuwa kila mtu ana uhuru wa kuhudhuria mikutano ya vyama tofauti ili kusikiliza ilani zao kutofautiana na vipi utekelezaji wake.

Hivyo aliwataka wananchi kutofanya makosa na badala yake kukichagua chama cha Mapinduzi ili kuona kwamba wanatekelezewa ahadi zilizomo ndani ya chama cha Mapinduzi.