NA NASRA MANZI

WAZIRI wa Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Balozi Ali Karume amewataka wafanyakazi wa Wizara hiyo, kuendelea kuwahimiza vijana kulinda na kuenzi utamaduni wao na kuacha kufuata tamaduni zisizofaa.

Akizungumza katika hafla ya kuagana na wafanyakazi na watendaji mbali mbali, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara huko Migombani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema utamaduni ndio utakaoweza kumsaidia kijana kujiletea mafanikio katika harakati zake za kujiinua kiuchumi.Pia alisema wataendelea kushirikiana katika masuala ya kazi pale panapohitajika  kwani lengo kuendeleza Taifa bora.

Sambamba na hayo aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuimarisha miundo mbinu ya michezo kwa vijana na wananchi kwa kujengwa viwanja mbali mbali katika Wilaya za Unguja na Pemba.

Alieleza jitihada nyingi zimefanywa na Serikali katika kuhakikisha michezo na Sanaa inakuwa na kuwapatia fursa vijana kuibua vipaji vyao.

Katibu Mkuu Wizara hiyo Omar Hassan King alisema utamaduni ,michezo na sanaa zilionekana kama burdani katika jamii, lakini kwa sasa vinawasaidia vijana kuinua uchumi.

Naibu Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Lulu Msham Abdalla alisema viongozi watakaobahatika kurejea, ni vyema  kuwatumikia vijana katika masuala ya  maendeleo.