NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema kazi kubwa inayotekelezwa na watendaji wa tume ya kitaifa ya kuratibu na udhibiti dawa za kulevya, imepunguza kwa kiasi kikubwa wimbi la uingizaji wa dawa hizo nchini.

Balozi Seif alieleza hayo alipofanya ziara ya kuwatembelea watendaji wa Tume ya kuratibu na udhibiti dawa za kulevya waliohama kutoka Kidongo Chekundu kutokana na ufinyu wa ofisi na hivi karibuni kuhamia kwenye jengo jengine lililopo Migombani.

Alisema Tume hiyo kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya dola wamefanya kazi nzuri ya kupunguza kasi ya uingizwaji wa dawa za kulevya hapa nchini.

Alifahamisha kuwa serikali imekaza kamba katika mapambano dhidi ya janga la dawa za kulevya ambalo ni hatari kwa afya za vijana wanaojihusisha na matumizi ya dawa hizo.

Balozi Seif alieleza kwa mujibu wa sheria nambari 9 ya mwaka 2009 ni kosa kwa mmiliki, mkaazi au msimamizi wa nyumba, jengo au mahali popote kuruhusu kutumika katika kutayarisha dawa za kulevya kwa ajili ya matumizi au kutengeneza, kuzalisha, kusambaza na kuuza.

Alieleza kwamba wapo baadhi ya watu wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya bila ya kujali kwamba bidhaa za dawa hizo zinaathiri jamii hasa vijana na kupoteza nguvu kazi ya taifa.

Balozi Seif aliwapongeza watendaji wa tume hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya licha ya kuzungukwa na mazingira magumu.

Awali mkurugenzi mkuu wa tume ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar, Kheriyangu Mgeni Khamis alisema watendaji wake wamepata faraja kwa kupata ofisi kubwa itakayokidhi kutekeleza vyema majukumu yao.

Kheriyangu alisema licha ya kuhamia kwenye jengo hilo kinachosubiriwa kufanyika ni marekebisho kwa mujibu wa maelekezo ya wakala wa ujenzi chini ya usimamizi wa wafanyakazi wahandisi wazalendo.

Mkurugenzi huyo alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana ya udhibiti wa uingizaji, usambazaji na uuzaji wa dawa za kulevya hapa nchini.