NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza wananchi kwa muamko wao wa kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na walimu, wanafunzi na wananchi wa Fujoni, baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ukumbi maalum wa kufanya mitihani kwa wanafunzi wa skuli hiyo.

Alisema ipo mifano katika maeneo mbalimbali hapa Zanzibar, wananchi wamekuwa mstari wa mbele kubuni, kujenga na kusimamia miradi inayolenga kuondosha changamoto zinazowakabili.

Makamu huyo alisema kuwa wananchi wanapokaa kitako kujadili na hatimaye kuamua kufanya mradi wa maendeleo inakuwa rahisi sana kwa mradi huo kutekelezeka hasa ikizingatiwa changamoto iliyopo ikiondoka ni kwa manufaa ya wananchi wote.

Alisema ujenzi wa ukumbi huo ambao ni miongoni mwa miradi ya kijamii iliyoibuliwa na shehia ya Fujoni pamoja na kwamba unagharamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), lakini umeibuliwa na wananchi.

Balozi Seif aliushukuru na kuupongeza uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), kwa miradi iliyomzawadia ya ujenzi wa majengo matatu ya kumbi za mitihani kama zawadi ya kumuunga mkono kutokana na utumishi wake katika jimbo la Mahonda.

Makamu huyo aliwataka wanafunzi wa skuli hiyo wajenge utamaduni mzuri wa kutunza rasilmali wanazojengewa na jamii ili zitumike na wanafunzi wa vizazi vya sasa na vile vijavyo.

Alisema serikali inawajibika kuwajengea mazingira bora Watoto ili waweze kukidhi vigezo vyao vya taaluma vinavyopaswa kwenda kwa kasi ya sasa ya sayansi na teknolojia ulimwenguni.

Katika hatua nyengine, Balozi Seif aliitumia fursa hiyo kwa kuwahimiza wananchi kushiriki kwenye zoezi la uchaguzi kwa amani na utulivu na kuwataka wazazi na wazee kuwaasa watoto wao kuepuka ushawishi vya baadhi ya wanasiasa.

“Asitokee kidudumtu akataka kukushawishini vijana zingatieni amani na epukeni kufanya vurugu ndani ya kipindi hichi, uchaguzi bila vurugu inawezekana”, alisema.