NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewataka vijana wanaoingia kwenye utumishi wa umma hapa nchini, wanatumia weledi katika kutekeleza majukumu yao.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na baadhi ya watendaji na viongozi waandamizi wa wizara za serikali na vikosi vya ulinzi kwenye hafla maalum aliyoiandaa kwa ajili ya kuwaaga baada ya kuamua kustaafu utumishi wa umma.

Kwenye hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil uliopo mjini hapa, Balozi Seif alisema mbali na weledi sifa nyengine inayomfanya mtumishi kuwajibika vyema ni uzalendo.

Alisema uzoefu unaonesha kuwa wapo baadhi ya watumishi ambao hawana muda mrefu tangu kupata ajira rasmi, wana haraka ya kutaka kubadilisha maisha yao katika kipindi kifupi.

Alisema tamaa ya watumishi walioajiriwa muda mfupi ya kutaka kubadilisha maisha mara nyingi huwaingiza watumishi wa namna hiyo katika balaa la kijilimbikizia mali kinyume na utaratibu.

Balozi Seif alisema cheo au kupanda daraja kwa mtumishi wa umma ni dhamana inayotokana na umahiri na jitihada za mtendaji, ambapo alisema kwa hivi sasa vijana wengi wameonesha uwajibikaji kiasi cha kuwepo kwa mabadiliko yaliyosaidia kupunguza umasikini.

Aliwapongeza viongozi na watendaji wa taasisi za umma hasa zile zilizo chini ya wizara aliyoiongoza kwa kujituma kizalendo kulikosababisha kupatikana mafanikio makubwa.

Mapema akitoa maelezo katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Shaaban Seif Mohamed alisema watendaji wa Ofisi hiyo wanajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya uongozi wake.

Shaaban alisema ofisi imefanikiwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara baina ya nchi na mataifa ya kigeni, mashirika na taasisi za kimataifa na kitaifa hali iliyotokana na ziara zake za nje pamoja na vikao na wawakilishi wa taasisi hizo.

Alisema uratibu mzuri wa shughuli za kukabiliana na maafa umesababisha uelewa wa taasisi na wananchi juu ya hatua za kujikinga na kukabiliana na maafa.