NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza waumini wa dini ya kiislam waliokosa kwenda kutekeleza ibada ya hijja mwaka jana kutokana na kuzuka kwa maradhi ya kuambukiza ya corona duniani.

Balozi Seif alitoa pongezi hizo wakati akizungumza na waumini wa dini hiyo wanaotarajia kwenda kutekeleza ibada hiyo hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakili, ambapo pia alitumia fursa hiyo kuaga baada ya kuitumia nafasi hiyo kwa miaka 10.

Alisema hadi sasa zipo baadhi ya nchi zinaendelea kuzuia raia wao kusafiri nje na kutoruhusu wageni kuingia kwenye nchi hizo kutokana na kuendelea kwa janga la ugonjwa huo.

Aliwataka mahujaji watarajiwa hao kutojisikia vibaya kutokana na kuzuka kwa ugonjwa na kwamba hata hivyo bado ulimwengu haujakaa salama kutokana na uwepo wa maradhi hayo.

Makamu wa Pili wa Rais, kupitia kundi hilo la mahujaji watarajiwa, aliwakumbusha wananchi kuzingatia umuhimu wa kutekeleza masharti yote yaliyowekwa na wataalamu wa afya katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.

Akitoa salamu kwa mahujaji watarajiwa hao, waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Hussein Mwinyi aliwaomba waendelee kuliombea dua Taifa ili livuke salama ndani ya kipindi hichi cha mpito cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Alisema wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wanachokihitaji kabla na baada ya uchaguzi mkuu ni kuona maisha yao yanaendelea kama kawaida bila ya wasi wasi katika muelekeo wa misingi ya amani na utulivu waliouzoea.

Dk. Hussein alisema endapo atapata ridhaa ya kuwatumikia wananchi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atakayoingoza itahakikisha kwamba changamoto zitakazowakabili waumini hao katika kwenda kutekeleza ibada hiyo itaangalia njia ya kusaidia kuzitatua.      

Mapema akitoa maelezo ya mtiririko mzima wa mwenendo wa mahujaji hao watarajiwa waziri wa Katiba na Sheria, Khamis Juma Maalim alisema Zanzibar ina taasisi 23 zinazosafirisha mahujaji kwenda kutekeleza ibada ya hijja nchini Saudi Arabia.