NA OTHMAN AME,

OMPRMAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya afya katika hospitali nchini ni ukombozi katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Alisema mfumo wa kuwasafirisha wagonjwa Tanzania bara na nje ya nchi, mbali ya kutumia gharama kubwa lakini pia ulikuwa ukihatarisha afya za wagonjwa.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati akiukabidhi uongozi wa hospitali ya rufaa ya Abdulla Mzee mashine ya uchunguzi wa maradhi ya moyo, figo, ini pamoja na vitakasa mikono vilivyotolewa na mfanyabiashara Said Nasser Nassor ‘Bopar’.

Alisema serikali itajitahidi kuzipatia vifaa tiba vinapatikana nchini ili kwenda sambamba na sera ya afya inayoelekeza kwamba huduma za afya zinawafikia wananchi kwa wakati mahali popote pale mijini na vijijini.

Aidha balozi seif alimpongeza mfanyabiashara huyo kwa uzalendo anaoendelea kuufanya kwa kuunga mkono sekta za elimu na afya nchini na kuwataka watendaji wa hospitali hiyo kuviangalia vyema ili vidumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.

Makamu wa Pili, aliwakumbusha watendaji wa afya hasa madaktari kuzingatia wajibu wa kusimamia sera ya matibabu bure iliyoasisiwa na chama cha Afro Shiray Party mara baada ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Aliutanabahisha uongozi wa Wizara ya Afya kwamba katika kuona  huduma za afya zinaimarika vyema na kuwafikia wananchi, haki za madaktari ikiwemo posho zao kutokana na  kufanyakazi katika muda wa ziara zinapatikana kwa wakati.

“Mcheza kwao hutunzwa. Hivyo tatizo hili lilokuwa kilio cha muda mrefu lazima lipungue au kuondoka kabisa kwani inashangaza huchukuwa karibu Miezi sita jambo lisilopendeza kabisa,” alisisitiza Balozi Seif.

Akitoa shukrani kwa niaba ya watendaji wa hospitali hiyo, Daktari Mkuu wa hospitali hiyo Dk. Haji Mwita Haji alisema kupatikana kwa mashine hiyo kutaongeza ubora wa huduma za afya zitakazotolewa hospitalini hapo.

Dk. Mwita alisema wananchi wanaofika hospitalini hapo kufanyiwa uchunguzi wa damu kutokana na maradhi mbalimbali, wakati mwengine hulazimika kusafirishwa kwenda Unguja au Tanzania Bara mazingira ambayo Familia za Wagonjwa hao hulazimika kutumia gharama kubwa wakati kipato chenyewe hakikidhi.