DORTMUND, Ujerumani
KIUNGO, Joshua Kimmich alifunga goli la ushindi na kuiwezesha Bayern Munich kuizidi kete Borussia Dortmund kwa kuilaza magoli 3-2 na kuebuka mabingwa wa SuperCup ya Ujerumani.
Bayern wameibuka na ubingwa huo licha ya hofu kuwa wachezaji wake wamechoka kutokana na kucheza mechi mfululizo kwenye kipindi kifupi.

Dortmund walikuwa wameongzwa 2-0 baada ya Corentin Tolisso na Thomas Müller kuwaweka mabingwa hao wa Ulaya kwenye uongozi.
Lakini, Erling Haaland aliwapa BVB goli la kwanza kisha akaongeza la pili ilipotimia dakika ya 55.
Ushindi huo wa Bayern umekuja baada ya kichapo cha magoli 4-1 walichopokea katika ‘Bundesliga’ mwishoni mwa wiki iliyopita mikononi mwa Hoffenheim.

Mechi hiyo ambapo mshambuliaji wa TSG Hoffenheim, Andrej Kramaric alipachika wavuni magoli mawili imezua tetesi kwamba Bayern sasa wanamuwinda mshambuliaji huyo raia wa Croatia.
Ripoti zinadai kwamba Bayern wanamtaka Kramaric awe msaidizi wa mshambuliaji wao, Robert Lewandowski ambaye alighadhabishwa na kushindwa huko wiki iliyopita.

Gazeti la kila siku la Ujerumani, Bild limeripoti kuwa mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo Hassan Salihamidzic aliwasiliana na wakala wa Kramaric baada ya kipigo hicho.
Kwa ushindi huo, Bayern inamaanisha kuwa sasa wameshinda mataji matano katika kalenda ya mwaka huu,
Walianza kwa kutwaa taji la ‘Bundesliga’, Kombe la Ujerumani, Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA Super Cup na SuperCup ya Ujrumani.

“Haikuwa rahisi hivyo haswa katika kipindi cha pili. Tuliongoza 2-0, lakini kisha tukafanya maisha yetu kuwa magumu,” alisema, kocha wa Bayern Hansi Flick. .
“La muhimu ni kwamba tulishinda mchezo. Kila kitu chengine tutahitaji kufanya vizuri siku ya Jumapili [dhidi ya Hertha].”
(ESPN).