LONDON, England

BERGMANN Johannesson mwenye miaka 17 anayecheza ndani ya klabu IFK Norrkoping amewekwa kwenye rada za mabosi wa Liverpool, Juventus na Manchester United wote wakiwania saini yake.

Ripoti zinaeleza kuwa Liverpool tayari wametuma wakala  ndani ya timu yake hiyo, ili kuweza kupata taarifa zake zaidi baada ya kuvutiwa na uwezo wa kinda huyo ambaye anacheza nafasi ya kiungo.

Nyota huyo anaaminika ndani ya kikosi cha IFK Norrkopinng na kwa msimu wa 2020/21, tayari amechangia jumla ya mabao 11 kwenye timu yake hiyo akifunga mabao matatu na kutoa pasi nane za mabao.

Ripoti zinaeleza kuwa mbali na Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England pia Manchester United wametuma wakala  ndani ya Norrkoping ili kuweza kuona uwezo halisi wa kijana huyo mdogo anayefanya makubwa ndani ya uwanja.

Kiongozi wa wakala ndani ya klabu ya IFK Norrkoping ,Stig Torbjornsen amesema kumekuwa na watu wengi ambao wanavutiwa na uwezo wa kinda huyo ambaye timu nyingi zimevutiwa naye.

 “Kuna timu nyingi ambazo zimeonesha kuvutiwa na huduma ya mchezaji wetu ila kwa sasa bado tunamhitaji kwani bado anakuja vizuri na miongoni mwa timu ambazo zinahitaji huduma yake ni pamoja na Liverpool,” amesema.