WASHINGTON, MAREKANI

WAGOMBEA wa urais nchini Marekani, Donald Trump wa Republican na Joe Biden wa Democratic, wamejitokeza katika vituo viwili tafauti vya televisheni, kila mmoja akimtuhumu mwenzake juu ya siasa za ndani na nje.

Katika kile kinachoonekana kama mdahalo baina yao, vituo viwili hasimu vya NBC na ABC nchini Marekani viliwaalika wagombea hao mahasimu pia kwa wakati mmoja kwa mahojiano ambayo yalirushwa moja kwa moja na kwa wakati mmoja usiku wa Alkhamis (Oktoba 15).

Watu wengi wameyachukulia mahojiano hayo kama duru ya pili ya mdahalo wa uso kwa uso kati ya Trump na Biden, ambao awali pia ulikuwa umepangwa kufanyika, lakini Trump alijitowa baada ya waandaaji kuamuwa ufanyike kupitia mtandao, kufuatia Trump kuuguwa COVID-19 wiki mbili zilizopita.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha ABC mjini Philadelphia, Biden alisema Trump hajayachukulia kwa umakini maradhi hayo, ambayo yameangamiza Wamarekani zaidi ya 217,000.

“Maneno ya rais yana uzito mkubwa, ama yakiwa mazuri au mabaya. Na pale rais anapokuwa havai barakowa ama anawafanyia dhihaka watu kama miye ambao tunavaa barakowa muda mrefu, utaona watu wanasema kwamba kumbe barakowa sio muhimu kiasi hicho,” alisema mgombea huyo wa Democratic ambaye anaongoza kwenye kura za maoni.