NA RAMADHANI KISSIMBA, PETER HAULE, DAR ES SALAAM

SERIKALI imezindua mradi wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vinne vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma, ili viwe na kiwango cha kimataifa, utakaogharimu shilingi bilioni 136.85.

Akizindua ujenzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango,  Doto James, amesema kuwa fedha hizo zimetolewa kama mkopo wenye masharti nafuu na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank) kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria katika maeneo hayo ya kimkakati.

‘’Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Wadau wa Maendeleo hususan Benki ya Uwekezaji ya Ulaya, kwa kukubali kufadhili mradi wa Viwanja vya Ndege vya kimkakati kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’Alisema  James.

Doto James, alieleza kuwa uboreshaji wa viwanja hivyo vya kimkakati unalenga kuvipa uwezo viwanja vya ndege vya mikoa ya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma, ili kutumia fursa nyingi zilizopo kwenye maeneo hayo.

Alisema hali hiyo itakuza uchumi ambao utakuwa chachu ya maendeleo katika Sekta ya Uchukuzi, Utalii, Kilimo na Anga katika mikoa husika na nchi kwa ujumla.

“Kukamilika kwa mradi huu kutaongeza uhakika wa kufikika, kurahisisha usalama, mawasiliano, na kuboresha biashara na nchi jirani na kuvifanya viwanja hivyo vitumike wakati wote kwa kuweka miundombinu ya taa na kuvipa hadhi ya Kimataifa ili ndege kubwa kama “Dreamliner” ziweze kutua” aliongeza James “Ni matumaini ya Serikali kuwa utekelezaji wa miradi hii utakuwa chachu ya maendeleo katika Sekta ya Uchukuzi, Utalii, Kilimo na Anga, katika mikoa husika na nchi kwa ujumla” alifafanua  James