LONDON, England

MKENYA Daniel Wanjiru, bingwa wa mbio za London Marathon mwaka 2017 amepigwa marufuku kushiriki riadha hadi mwaka 2023 kwa kosa la kutumia dawa za kusimumua misilu.

Awali, Wanjiru alipigwa marufuku kwa muda hadi Aprili lakini amekanusha madai kwamba alitumia dawa zilizokatazwa na kuomba kufungua kesi mahakamani.

Shirika la kukabiliana na dawa ya kusisimua misuli duniani (AIU) sasa limethibitisha kwamba marufuku ya mwanariadha huyo (28), , kuwa itaendelea hadi Desemba 8, 2023.

Msimamizi wa Wanjiru amesema wamekatishwa tamaa na uamuzi huo na wanafikiria kukata rufaa kupitia mahakama ya michezo ya usuluhishi wa mizozo.

“Wataalamu wetu wametoa maelezo mazuri ya kiwango cha damu na wameonesha uwezekano wa chini wa utumiaji wa dawa za kusisimua misuli – ikilinganishwa na ilivyoelezwa na Shirika la Riadha Duniani,” taarifa hiyo imeeleza.

“Tunasisitiza kwamba hakuna chembe za dawa yoyote iliyokatazwa ambayo imewahi kupatikana na tunaamini kwamba Daniel hana hatia.”

Taarifa zilizochapishwa na shirika la AIU inaeleza kwamba sampuli ya Wanjiru inaonesha kiwango fulani cha seli nyekundu za damu jambo ambalo halina maelezo yoyote.

Alifanyiwa vipimo mara 16 kati ta Aprili 2017 na 2019. Katika vipimo vyake vya 14 – Machi 9, 2019 – alionyesha kiwango cha juu cha hemoglobini.

Ilihitimishwa kwamba mabadiliko ya viwango vya damu wakati anafanyiwa vipimo “hakukuweza kuelezewa kwa sababu yoyote ile zaidi ya udanganyifu wa damu”.

Jopo hilo lilisema “kuna uwezekano mkubwa” dawa iliyopigwa marufuku au kitu kingine kisichoruhusiwa kilitumika.

Wanjiru alishinda mbio za Amsterdam Marathon mwaka 2016 na kumaliza wa nane na wa 11 katika mbio za London Marathon mwaka 2018 na 2019 mtawalio.