NA MWANAJUMA MMANGA

ILI kukabiliana na mahitaji ya damu, benki ya damu salama Zanzibar, wiki ijayo inatarajia kufanya bonanza maalum la kuchangia damu litakalofanyika Chakechake, kisiwani Pemba.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, Meneja Masoko na Uhusiano wa benki hiyo, Bakari Omar Magarawa, alisema wanatarajia bonanza hilo litakalodhaminiwa na kampuni ya Bopar Interprises anatarajia litaongeza hamasa ya wananchi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji tiba ya damu.

Alisema kuwa hivi sasa benki inaendelea na uhamasishaji wa wananchi kuchangia damu kwa hiyari kupitia mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu inayoendelea.

Magarawa alisema, katika wiki liyopita benki hiyo ilikusanya damu chupa 350 kupitia mabonanza mawili yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi wa tisa huko visiwani Pemba.

Alisema na kwa upande wa Unguja, bonanza kama hilo lilifanyika Kisonge wiki iliyopita na kufanikiwa kukusanya chupa 400 huku mahitaji ya damu kwa mwezi yakiwa ni zaidi ya chupa 1,350.

Alifahamisha kuwa wanaendelea kuzichunguza ili baadae zitasambazwa katika vituo vya afya ikiwemo hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa Unguja, hospitali ya Adallah Mzee Pemba pamoja na vituo vya afya vinavyotoa huduma za uzazi.

“Tunashukuru kipindi hiki tuna akiba nzuri na ya kutosha na tunaamini damu tuliyoipata itatusaidia katika vituo vyetu vya afya kwa wagonjwa, akinamama wajawazito na wawanaopata ajali,” alisema.

Alisema hapo nyuma walikuwa na uhaba wa damu kutokana na kupunguza harakati za uchangiaji damu kutokana na kuibuka kwa maradhi ya Covid 19 lililoikumba dunia nzima.

Hivyo ameitaka jamii kuendelea kuchangia damu na kupima afya zao ili iweze kusaidia na kuhakikisha kunapatikana damu ya kutosha.

Naye miongoni mwa wachangiaji damu Salum Hussein Idarous, alisema hii ni mara yake ya kwanza kuchangia damu kutokana na ushauri aliopatiwa baada ya kugundulika kuwa na damu nyingi.

“Nilikuwa nasumbuliwa sana na kichwa, ndipo baada ya uchunguzi daktari alinambia kuwa inachangiwa kuwa na damu nyingi ndipo nilipoamua kujitolea na nitaendelea kufanya hivyo kwa afya yangu na wagonjwa wengine,” alisema Idarous.