NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

KAMATI ya Sera na Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imesema imeridhika na mwenendo wa viashiria vya uchumi mpana ambavyo vimeendelea kuwa imara na kubakia ndani ya malengo yaliyokubalika kikanda.

Alisema kasi ya mfumuko wa bei imeendelea kuwa katika kiwango cha tarakimu moja cha wastani wa asilimia 3.3 kwa mwezi Julai hadi Agosti mwaka huu.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jijini hapa, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga alisema kamati hiyo ilifanya mkutano wa kawaida Oktoba 5, mwaka huu ili kuthamini hali ya sasa ya mwenendo wa uchumi na mwelekeo wake, ambapo hukutana mara moja kila baada ya miezi miwili.

Alisema kamati hiyo imeridhika kuwa uchumi unaendelea kuimarishwa licha ya athari za janga la virusi vya corona kwa kuzingatia viashiria mbali mbali vya uchumi unaotarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 mwaka huu.

Alieleza matarajio ni kuwa mfumuko wa bei utaendelea kubakia kati ya asilimia 3 hadi 5 mwaka 2020/2021, kama ilivyokadiriwa awali.

Gavana huyo alisema matarajio hayo yanatokana na mwenendo mzuri wa uzalishaji na ugavi wa mazao ya chakula kwa kiwango cha kutosha nchini, utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, wastani wa bei za mafuta kuendelea kubakia katika viwango vya chini pamoja na sera madhubuti za fedha na kibajeti.

Aidha alifafanua kuwa, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kubakia katika viwango vya juu, zaidi ya dola za Marekani bilioni 5, kiasi ambacho kinatosheleza uagizaji bidhaa na huduma na uhamisho mali nchi za nje imeendelea kupungua kufuatia kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi, hususani dhahabu na korosho.

Vile vile kutokana na utekelezaji na usimamizi thabiti wa sera ya fedha, hali ya ukwasi katika uchumi imeendelea kutosheleza mahitaji mbali mbali ya shughuli za kiuchumi na kusababisha kupungua kwa viwango vya riba za mabenki.