MUNICH, Ujerumani
KOCHA wa Werder Bremen, Florian Kohfeldt, amezungumzia kuhusu hali tete ya kifedha katika klabu hiyo ya Ujerumani, ambayo imeshindwa kumpata mbadala wa mchezaji muhimu aliyeondoka, Davy Klaassen.

Klaassen amerejea katika klabu ya Ajax Amsterdam katika siku ya mwisho ya uhamisho kwa kitita cha euro milioni 11.
Pia wanalenga kumuuza, Milot Rashica kwa Bayer Leverkusen hali ambayo hata hivyo haikuweza kufanikiwa.

“Hatujafikia lengo letu la uhamisho kwa mtazamo wetu wa kimichezo”, Kohfeldt, alisema baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya St Pauli Hamburg.
“Lakini Werder Bremen imo katika hali mbaya ya kifedha. Kila mmoja ni lazima atambue hilo, na kila mmoja ni lazima apambane”.

Mabingwa hao wa zamani wa Bundesliga wameathirika pakubwa na janga la virusi vya ‘corona’ na uwanjani waliepuka tu kushuka daraja msimu uliopita katika mpambano wa mchujo dhidi ya timu ya daraja la pili.

Walianza msimu mpya kwa ushindi mara mbili kutoka michezo mitatu, lakini, Kohfeldt, alisema, wanapaswa kuimarika kutokana na hali ya juu ya kitisho katika michezo.(AFP).