LONDON, England

MSHAMBULIAJI Dominic Calvert-Lewin amechaguliwa kuwa mchezaji bora ndani ya Ligi Kuu England kwa mwezi Septemba, baada ya kufunga mabao matano na kuifanya timu yake ya Everton kuwa vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 12.

Nyota huyo anayekipiga ndani ya Everton jitihada zake zimeonekana ndani ya Septemba akiwapoteza Harry Kane wa Spurs, Sadio Mane wa Liverpool na mchezaji mwezake ndani ya Everton James Rodriquez.

Nyota huyo mwenye miaka 23 alifunga bao pekee la ushindi kwenye mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu England walipocheza na Totteham kisha aliifungia (hat trick), timu yake ilipocheza na West Brom Uwanja wa Goodison park iliposhinda mabao 5-2.

Pia alifunga kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Crystal Palace siku saba baadaye na kufanya awe bora ndani ya Everton ambayo imeanza kwa kasi msimu wa 2020/21.

Chini ya kocha Mkuu, Carlo Ancelotti imeshinda mechi zote nne za Ligi Kuu England, na baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora kwa mwezi Septemba, alitumia ukurasa wake wa Twitter kuwashukuru mashabiki na wadau wake.

“Msimu wa kipekee na wenye nguvu za kutosha kwetu, ninawashukuru wachezaji wenzagu pamoja na wale ambao wamenipigia kura na kunichagua, asante sana watu wazuri kwa kunipigia kura na kunichagua,” amesema.