ACCRA, Ghana

ADHABU ya kutojihusisha na shughuli za soka maisha dhidi ya rais wa zamani wa shirikisho la soka nchini Ghana Kwesi Nyantakyi, imepunguzwa hadi miaka 15 baada ya rufaa iliyopelekwa kwenye mahakama ya kimichezo (CAS).

Mjumbe wa baraza la FIFA na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Afrika Nyantakyi, alifungiwa maisha na FIFA mwezi Oktoba mwaka 2018 kwa kuvunja sheria zinazopiga marufuku vitendo vya rushwa.

Alinaswa kwenye kamera akipokea kiasi cha dola za Marekani 65,000 kutoka kwa mwanahabari wa uchunguzi .

”Kwesi Nyantakyi amepigwa marufuku kujihusisha na shughuli zozote zinazohusu michezo kitaifa na kimataifa kwa miaka 15, kuanzia tarehe 29 mwezi Oktoba mwaka 2018,” Cas iliiambia BBC Sport Africa.

Faini ya awali ya raia huyo wa Ghana ilikuwa dola za kimarekani 550,000 pia imepunguzwa mpaka dola 110,000 baada ya uamuzi wa Mahakama ya michezo mwezi Aprili ambao umejulikana hivi karibuni.

Nyantakyi, ambaye alieleza shauku yake ya kusafisha jina lake siku chache baada ya uamuzi wa kamati ya nidhamu ya FIFA, alikata rufaa kwenye mahakama ya michezo Cas mwezi Disemba mwaka 2018.

Video ya kigogo huyo wa zamani akichukua mlungula ilichukuliwa na mwanahabari Anas Aremeyaw Anas wa kitendo cha uchunguzi cha BBC, Africa.