TAKDIRI ALI, MAELEZO ZANZIBAR

VIJANA Nchini wametakiwa kuendelea kukithamini na kukichagua Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni wa mwezi huu, ili chama hicho kiendelee kuleta maendelo kwa wananchi wake.

Hayo yameelezwa na Kiongozi Mkuu wa Harakati za Vijana ndani ya Mkoa  wa Magharibi, Thuwaiba Jeni Pandu, katika ziara ya kuhamasisha vikundi vya wajasiriamali, boda boda ,wauza samaki na wasanii huko Mfenesini Unguja.

Kiongozi huyo alisema Serikali ijayo kupitia CCM itazidi kuweka utaratibu mzuri kwa makundi hayo utakao wapelekea kufanya kazi kwa ufanisi na kujipatia kipato.

Ameahidi kuwa Serikali ya awamu ya nane itaweka mfumo madhubuti wa kuwaongezea mitaji Wajasiriamali wadogo wadogo pamoja na kuwapatia usajili rasmi waendesha boda boda, ili kukuza biashara zao na kuiwezesha serikali kukusanya mapato.

Aidha amewasihi Vijana wasikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa wasiopenda maendeleo ya nchi na kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo hapa nchini.  

Nao viongozi wa wanavikundi hivyo wameomba kutembelewa mara kwa mara, ili kuweza kufahamika matatizo yao na kupatiwa ufumbuzi wa haraka sambamba na kuahidi kuendelea kukipa ridhaa Chama Cha Mapinduzi ili kiendelee kuongoza dola kwa maslahi bora ya wananchi wake.