NA MWAJUMA JUMA
CHAMA Cha Michezo kwa Watu Wenye Ulemavu wa Viungo Zanzibar kimo katika mchakato wa kutaka kuunda timu Pemba ili kuongeza idadi ya timu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwenyekiti wa chama hicho Hassan Haji Silima alisema hatua hiyo ni moja ya mikakati yao ili kuweza kupitisha katiba ya shirikisho la mchezo huo visiwani Zanzibar.
Alisema hivi sasa chama chao kimo katika hatua za mwisho za kumalizia kupitisha katiba ya shirikisho hilo, lakini ili kuwa na sura ya shirikisho wameona ni vyema wakawa na timu kutoka Pemba.
Alisema mchakato wa kupatikana timu hizo unaendelea vizuri ambapo mpaka sasa wamepata wachezaji 12 na wanatarajia kuongeza wanne ili kutimia timu mbili kamili.
“Mpaka sasa tuna timu tatu za watu wenye ulemavu wa viungo vya miguu na mikono na zote zipo Unguja, kuanzishwa timu hizo kutaongeza idadi ya timu Unguja na Pemba”, alisema.
Alifahamisha kwamba mpaka sasa wana rasimu ya katiba na mara zitakapopatikana timu hizo wataipeleka kwa Mrajisi ili kuipitia na kuipitisha.