SANTIAGO, CHILE

MAANDAMANO dhidi ya kukosekana usawa nchini Chile yamekuwa ya vurugu,ambapo waharibifu walichoma makanisa mawili, na kuharibu moja kati yao.

Waandamanaji walioficha nyuso zao, walishambulia makanisa hayo, na kuyachoma moto katika maeneo ya mji mkuu wa, Santiago.

Tukio hilo lilitokea baada ya maelfu ya watu kukusanyika katika uwanja wa kati wa Santiago, kuadhimisha mwaka mmoja wa maandamano makubwa ambayo yalisababisha zaidi ya watu 30 kufa na maelfu kujeruhiwa.

Lakini mkutano huo uliotarajiwa kuwa wa amani uligeuka na kuwa ghasia na uporaji baada ya kufikia majira ya usiku.

Kutokana na hali hiyo, Polisi walilazimika kurusha mabomu ya machozi na maji ya kuwasha ili kuwatimua waandamanaji hao.

Waandamanaji pia waliwataka watu kupiga kura kupendelea katiba mpya katika kura ya maoni itakayopigwa wiki ijayo.

Waandamanaji walilalamikia katiba ya Chile, ambayo inaanzia miaka ya utawala wa jeshi baada ya Jenerali Augusto Pinochet kutwaa madaraka mnamo mwaka1973.     Maandamano ya mwanzo yalifanyika mnamo Oktoba mwaka jana nchini Chile na yalifanyika karibu kila siku, lakini yalipungua kwa kiasi kikubwa kutokana na janga la maradhi ya corona.