OTTAWA, CANADA

BALOZI wa China nchini Canada Cong Pei-wu ameionya serikali ya Canada, dhidi ya kuwapa hifadhi wakaazi wa Hong Kong, walioikimbia sheria ya usalama inayokosolewa vikali, iliyowekwa na utawala wa Beijing kwenye jimbo lake hilo.

Balozi Cong Pei-wu alisema kuwa waandamaji wanaounga mkono demokrasia huko Hong Kong, ni wahalifu wasiostahiki hifadhi, hivyo ameonya kwamba kuwapa hifadhi watu kama hao, kutachukuliwa kuwa ni kuingilia mambo ya ndani ya China, jambo ambalo halikubaliki.

Cong alisema, endapo Canada inawajali wakaazi 300,000 wa Hong Kong wenye paspoti za Canada, na pia kampuni zake zilizoko Hong Kong, basi inapaswa kuunga mkono juhudi za China, kupambana na kiel alichokiita “uhalifu,” badala ya kuwapa hifadhi watu hao.

Canada imekuwa ikiwapa hifadhi viongozi wa maandamano ya wanafunzi kutokea Hong Kong, na wale wanaoikimbia sheria mpya ya usalama, iliyoanza rasmi kutumika tarehe 30 Juni mwaka huu.