BEIJING,CHINA

WAENDESHA mashitaka wa China wamesema wamewakamata rasmi wanaharakati 12 wanaopendelea demokrasia Hong Kong waliokamatwa kwa tuhuma za kuingia Taiwan kinyume cha sheria.

Tangazo hilo limetolewa na maofisa wa Shenzhen katika jimbo la Guangdong,lililo jirani na Hong Kong.

Vyombo vya habari vya Hong Kong vinasema wanaharakati hao 12 wenye umri wa kati ya miaka 16 na 32 walikamatwa na maofisa wa ulinzi wa pwani wa China mwishoni mwa mwezi Agosti wakijaribu kuingia Taiwan kwa kutumia boti.

Vyombo vya habari vinasema wengi wao walikuwa wameachiliwa kwa dhamana baada ya kukamatwa au kushitakiwa na mamlaka za Hong Kong kuhusiana na maandamano tangu mwaka jana.

Familia za waliokamatwa zinasema bado hazijapokea taarifa zozote kuhusiana na wanaharakati hao baada ya kusafirishwa kwao hadi kizuizini.

Familia hizo pia zinasema wanaharakati hao 12 walizuiliwa kuzungumza na mawakili.

Waangalizi wanasema maandamano ya kuipinga China huenda yakaongezeka baada ya kutangazwa kukamatwa kwa wanaharakati hao.