NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuzinduliwa kwa Chuo cha Amali cha Daya Mtambwe na cha Kisongoni Makunduchi ni fursa ya kuimarisha sekta ya ajira kwa vijana.

Dk. Shein alieleza hayo jana huko Daya Mtambwe, alipokuwa akifungua chuo hicho na chuo cha Amali cha Kisongoni Makunduchi, hafla iliyohudhuriwa na viongozi kadhaa wa vyama vya siasa na serikali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Alisema kuwa vyuo hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana na kuwataka vijana wasivunjike moyo, waendelee kusoma na faida yake watakuja kuiona baadae.

Dk. Shein alisema kuwa matajiri na mabilionia wengi hapa nchini na hata nje ya nchi wengi wao utajiri wao unatokana na ujasiriamali.

Alieleza kuwa kuridhika na mafunzo mapya ambayo yameongezwa katika masomo kwenye vyuo vya amali yakiwemo masomo ya uvuvi na kilimo ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuufikia uchumi wa buluu.

Kutokana na ombi la uongozi wa Wizara hiyo ya Elimu na Mafunzo ya Amali kutaka eneo kwa ajili ya mafunzo ya kilimo, Dk. Shein aliahidi kuwapa eneo hilo huku akiwaeleza kuwa kwa upande wa bahari wanaruhusika kuendelea na mafunzo.

Aidha, alisema vituo vya mafunzo ya amali ni fursa ya kuwapa mafunzo ya ujuzi wa fani za ufundi vijana na wengi kati ya wanaomaliza katika vituo hivyo wanaendelea na maisha yao kwa makubwa.

Sambamba na hayo, aliupongeza uongozi wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali huku akisisitiza kwamba Chuo hicho kipelekwe walimu wenye sifa ili maendeleo zaidi yapatikane kama yalivyopatikana katika vyuo vyengine.

Kwa upande wake waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Risiki Pembe Juma alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa jitihada zake za kuhakikisha anatekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 ambapo aliahidi kukijenga chuo hicho.