ARUSHA, TANZANIA

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), imepoteza dola zaidi ya bilioni 37 kutokana na kusimama kwa baadhi ya shuhguli tangu ulipotokea mripuko wa janga la maradhi ya corona.

Ofisa mkuu wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Peter Mathuki alisema tangu janga la virusi vya corona lilipotokea nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepoteza zaidi ya dola bilioni 37, kutokana na kukwama kwa shughuli nyingi za kibiashara.

Mathuki alizitaka nchi sita zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kushirikiana ili kutatua mizozo ya mipakani inayoathiri biashara katika ukanda huo.

Katika siku za hivi karibuni, madereva wa malori ya mizigo wanaotoka Kenya kwenda Uganda, wanalalamika vikali kuhusiana na masharti makali yaliyopo mipakani.

Masharti hayo yanayowalazimisha kukaa mpakani kwa zaidi ya wiki moja, hali inayoathiri bidhaa nyingi haswa vyakula, kando na kulemaza shughuli za kibiashara katika mataifa husika.

Mathuki alisema tayari baraza hilo limewaarifu mawaziri husika kutoka nchi sita wanachama wa Jumuiya hiyo, ili kutafuta suluhisho la tatizo hilo.

Aidha, alisema, sekta ya utalii katika kanda ya Afrika Mashariki imeathirika zaidi na kuchangia asilimia 92 ya hasara ya kibiashara katika kandahiyo.