NA ZUHURA JUMA, PEMBA

KAMATI ya kupinga vitendo vya udhalilishaji ya Wilaya ya Wete imelipongeza Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia la Wanawake na Watoto Wilaya hiyo, kwa juhudi wanazozichukua katika kufuatilia na kusimamia kesi za udhalilishaji.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu tawala Wilaya hiyo, Mkufu Faki Ali wakati, akipokea ripoti ya utekelezaji wa kupiga vita vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu.

“Zamani tulikuwa tunapokea malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi kuhusu utendaji kazi wa dawati la kijinsia la Wete, lakini kwa sasa malalamiko hayo yamepungua kutoka na utendaji mzuri uliopo sasa, wanahitaji pongezi kwa hatua iliyofikiwa”, alisema Katibu huyo.

Wajumbe waliohudhuria mkutano huo wa kuwasilisha ripoti, wameishauri Serikali kuingalia tena upya Sheria ya Mtoto ya mwaka 2011 ya Zanzibar, kwani imekuwa ni sababu ya kuongezeka kwa
vitendo vya udhalilishaji na hasa kwa vile hakuna mahakama ya watoto na baadhi ya watoto kukindhana na sheria.

“Kwa vile mtoto hata akifanya kosa la udhalilishaji hafungwi, wamekua wakirudia vitendo hivyo kutokana na kuwa wengi wao ni watoto wenye umri mkubwa kuanzia miaka 16 hadi 17, hiki ni kikwazo kikubwa kinachotuumiza vichwa”, walisema.