NA TATU MAKAME

NAIBU Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Maryam Ramadhan Hamoud, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeweka sheria ya Diaspora, ili kuweza kurahisisha kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo kiuchumi na kijamii.

Aliyasema hayo, alipokuwa akikabidhi vifaa vya elimu kwa uongozi wa skuli ya msingi Kikungwi Wilaya ya Kusini Unguja, vilivyotolewa na taasisi ya Ahas Group kutoka Denmark kupitia wazanzibar wanaoishi nje ya nchi (Diaspora).

Alisema kuanzishwa kwa sheria hiyo kumewatia moyo wazanzibar wanaishi nje ya nchi kwa kusaidia ndugu zao wa Zanzibar, jambo ambalo limeweza kusaidia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo sekta ya elimu.

Aidha, alisema kuwa, yote hayo inaonesha kuwa Diaspora wamekuwa wakiendelea kuunga mkono juhudi za serikali zinazoendelezwa na uongozi wa serikali chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

‘Serikali imekuwa ikiwajali wananchi wake na ndio maana inafanya kila mbinu ikiwemo kuwatatulia wananchi changamoto zinazowakabili katika mitaa yao pamoja na jamii kwa ujumla’alisema.