NA ABOUD MAHMOUD

WANACHAMA wa Chama cha Mpainduzi, wametakiwa kuhakikisha wanatumia haki yao ya msingi ya kupiga kura ili kukiweza chama hicho kuendelea kuleta maendeleo nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa na Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete wakati akizungumza na wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na Udiwani wakiwemo wa viti maalum wa mkoa wa Mjini Magharibi katika ukumbi wa CCM Amani mkoa.

Kikwete alisema ni vyema wana CCM kuendeleza umoja wao ambao una lengo la kuhakikisha chama hicho kinarudi madarakani kwa kishindo.

Alisema anaamini ushirikiano wao ndio utakaosababisha majimbo yote tisa ya Mkoa wa Mjini Magharibi kuchukuliwa na CCM.

“Ushirikiano na jambo zuri sana na kama mtaendelea nao basi nina matumaini makubwa majimbo yote ya Mkoa wa wa Mjini yatachukuliwa na CCM,” alisema.

Rais mstaafu ambae pia ni Mwenyekiti mstaafu wa CCM alisema katika uchaguzi hususan wa ngazi za juu wakati mwengine hutokea mfarakano unaotokana na kushindwa kwa mgombea katika nafasi hizo.

Hivyo aliwataka wagombea hao kuendeleza mashirikiano waliyonayo kuondosha makundi ili kuhakikisha viongozi waliopata nafasi hizo wanashinda na wanashirikiana na wenzao katika kuunda Serikali.

“Tusikasirike umekosa mwaka huu jipange kwa mwaka 2025 ingia tena kwenye mchakato unaweza kupata mimi mbona niligombania Urais na sikupata na sikukasirika namshkuru Mungu nilipoingia tena nimefanikiwa,” alifafanua.

Mstaafu huyo aliwapongeza viongozi wote wa Mkoa wa Mjini na Mkoa wa Amani kichama kwa kuandaa mkutano huo ambao utasaidia kuleta manufaa katika kipindi cha uchaguzi.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mjini, Juma Faki hapo aliahidi kuendeleza mashirikiano yao na kuzifanyia kazi nasaha walizopewa katika kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo.

Alisema mpaka hivi sasa watia nia wa majimbo na wale wa viti maalum wamekua wakishirikiana katika kuomba kura kwa ajili ya kuhakiksha CCM inabaki madarakani.