Atoa majibu hoja nzito za muungano, kiuchumi
Asema Mwinyi ni mtu sahihi kuiongoza Zanzibar
NA KHAMISUU ABDALLAH
MGOMBEA wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, amesema muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndio uliowezesha kujenga taifa lenye nguvu na uhuru wa kweli.
Dk. Magufuli aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia wanaCCM na wananchi wa Zanzibar katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Mnazimmoja.
Alisema taifa la Tanganyika na Zanzibar yaliamua kuungana na kuunda taifa jipya la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na ushujaa wa waasisi marehemu Julius Nyerere na marehemu mzee Abeid Amani Karume.
Alisema muungano huo umeifanya Tanzania kuwa nchi pekee barani Afrika isiyokuwa na kurithi mipaka iliyowekwa na wakoloni na taifa liloundwa na wananchi wenyewe wa Zanzibar na Tanganyika kwa hiari yao.
Dk. John ambae pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa alisema muungano wa Tanganyika na Zanzibar sio wa kulazimishwa, bali ulitokana na maono ya wasisi hao hususan mtangamano wa bara la Afrika, ukaribu wa kijiografia kati ya Tanganyika na Zanzibar, mahusiano ya kindugu baina ya wazanibari na watangayika, uhusiano wa vyama vilivyopigania uhuru wa nchi mbili ikiwemo TANU na ASSP.
“Ukimsikia mtu anasema Muungano wetu wa kulazimishwa basi ni uzushi na hafahamu historia ya nchi yetu na hafai kupewa dhamana ya kuliongoza taifa letu na haya yamefanikiwa kwa sababu ya Muungano wetu”, alibainisha.
Hata hivyo, Dk. Magufuli alisema katika mashirikiano yao kati ya Zanzibar na Tanzania bara Tanzania ni Taifa pekee ambalo halikuyumbishwa na maradhi ya korona kwa kukataa kupokea maelekezo ya kufunga mipaka na kuwafungia wananchi kufanya shughuli zao.
“Hii imetudhirishia kuwa Tanzania ni taifa huru lenye kuamua mambo yake wenyewe bila ya kushawishiwa na mtu yoyote kwa manufaa yetu wenyewe tulikataa kuwa kama dodoki kavu,” alisema.
Mbali na hayo Dk. Magufuli alibainisha kwamba Tanzania na Zanzibar ya leo sio ya mwaka 1964 kwani mafanikio makubwa yamepatikana ikiwemo kuimarika kwa uchumi na Taifa la Tanzania kufikia uchumi wa kati hiyo inatokana na sababu ya Muungano imara.
Alisema yapo maneno yanayotolewa na baadhi ya watu kuwa Zanzibar haipati mapato au kudhulumiwa na kubainisha kwamba ipo miradi mikubwa ya Zanzibar iliyokopewa fedha na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema katika kipindi cha miaka 40 jumla ya ya fedha taslim shilingi trilioni 2.3 zimekopwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya miradi mikubwa ya maendeleo Zanzibar pekee ikiwemo mradi wa ujenzi wa miundombinu ya maji, ujenzi wa skuli, ujenzi wa miundombinu ya usafiri Terminal III.
Mgombea huyo alipongeza awamu zote za serikali mbili hasa, Dk. Ali Mohammed Shein katika kushirikiana kuulinda Muungano na kutekeleza ilani ya mwaka 2015/2020 kwa kiwango kikubwa.
Alisema, Zanzibar imepata mafanikio mengi katika kipindi cha Dk. Shein ikiwemo kudumisha Mapinduzi, kuimarisha amani ya nchi kuogeza uchumi wa Taifa na kuongeza thamani ya pato la taifa kutoka trilioni 2.4 mwaka 2015 hadi trilioni 3.1 mwaka 2019.
Kwa upande wa makusanyo ya mapato alisema katika uongozi wa Dk. Shein mapato yameongezeka kutoka bilioni 428.5 hadi 748.9 huku mfumuko wa bei umetoka asilimia 5.7 hadi asilimia 2.7 na kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 7.
Eneo jengine, alisema ni kukuza sekta ya utalii na kuongeza idadi ya watalii kutoka watalii 294243 mwaka 2015 hadi watalii 538264 mwaka 2019 na kuvuka lengo lilowekwa kwenye ilani ya mwaka 2015 ya kutembelewa na watalii 5,000,000.
Hata hivyo, akizungumzia sekta ya kilimo alisema Dk. Shein ameisimamia sekta hiyo ikiwemo kuongeza uzalishaji wa zao la karafuu kutoka tani 3321.7 hadi tani 8277 na mpunga kutoka tani 281,226 hadi tani 404,285.
Mbali na hayo, alisema pia ameweza kujenga miundombinu ya barabara za lami zenye urefu wa kilomita 159.14 ikiwemo barabara ya Ole- Kengeja, ununuzi meli ya abiria ya Mv. Mapinduzi 11, Mt Ukombozi, Ujenzi wa soko la Kisasa katika bandari ya Malindi, ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume na ujenzi wa kiwanja cha Kigunda.
Maeneo mengine alisema ni uboreshaji wa huduma za jamii ikiwemo kuongeza skuli za msingi kutoka 260 hadi 381 sambamba na ujenzi wa skuli za umahiri kwa wanafunzi wa sayansi na hisabati na uchimbaji wa visima 250 kwa Unguja na Pemba.
Akimzungumzia mgombea wa urais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema katika miaka 20 ya utumishi wake anamtosha kuwa Rais wa Zanzibar kwani ana moyo wenye uvumulivu na wakipekee.
“Dk. Hussein Mwinyi ni chaguo sahihi katika kuiongoza Zanzibar kwani ameshika nafasi mbslimbali na kikana makini muadilifu na mchaap kazi asiependa uzembe,” alisema.
Mbali na hayo alisema, Dk. Mwinyi anasifa kubwa ya kupeperusha bendera kwani ni kijana aliyezaliwa baada ya Muungano na Mapinduzi na mtu sahihi ambae anafahamu nini wazanzibari wanataka.
Aliwahikishia wazanzibari kwamba endapo watamchagua basi atashirikiana nae katika kuijenga Zanzibar na kuhakikisha kwamba mafuta na gesi itakayopatikana Zanzibar ni mali ya wazanzibari wenyewe.
“Zanzibar inahitaji mtu makini kusimamia masahi ya wazanzibari hata katika suala la dhulma, ufisadi, na naamini Mwinyi atakapoingia madarakani ataendeleza falsafa yake ya kusikiliza shida za wananchi,” alimuomba.
“Tumepanga kujenga nchi ya kufuata ilani na kushirikiana pamoja katika Mapinduzi ya kiuchumi, ikiwemo uchumi wa Viwanda na bahari kuu ili kuona watanzania wananufaika na uchumi wao,” alisema.
Sambamba na hayo aliwasisitiza wananchi kudumisha amani na utulivu wa nchi yao ili waweze kuendelea kupata maendeleo na kukataa mipango inayopangwa na baadhi ya maslahi ya watu binafsi.
“Uchaguzi huu ni muhimu kuchagua watu wenye maslahi ya kweli tunawaomba sana wananchi mtuchague viongozi wa CCM ili tuendelee kulinda, Muungano, Mapinduzi na kuitetea wanyonge,” aliwaomba.
Dk. Magufuli aliwapongeza wazanzibari kwa kumpa mapokezi makubwa na kuahidi kuwa mapokezi hayo yamempa deni kuwafanyia kazi wazanzibari na Tanzania kwa ujumla.
Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuongoza vyema serikali na kuongoza CCM kwa upande wa Zanzibar na kuwaleta maendeleo kwa asilimia kubwa.
Aliwasisitiza watanzania kuendelea kushikamana na kuilinda umoja wao ili waendelee kuwa taifa huru na kuahidi kutatua kero ndogo ndogo zilizokuwepo katika muungano wao.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa imetekeleza kwa vitendo ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa kiwango kikubwa.
Alisema, wananchi wa Zanzibar wapo tayari kuwapa kura viongozi wa CCM kwani wana matumaini makubwa kwao na misingi mikubwa ya kuendeleza Muungano na Mapinduzi katika misingi ya wasisi Mwalimu Julias Nyerere na mzee Karume.
Nae, Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi akichaguliwa atahakikisha anayaenzi Mapinduzi na Muungano wao kwa nguvu zote.
Alisema CCM katika kampeni zake imekuwa ikinadi sera zake kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi wa Zanzibar.
Aidha alisema suala la uchumi wa bhari linawezekana kutekelezwa kutokana na kuwepo kwa mipango mizuri na sheria katika ilani ya uchaguzi yam waka 2020/2025.
Akizungumzia msekta ya mafuta na gesi alisema itaendelea kuwa ni mali ya wazanzibari kwani tayari imeshapitishwa sheria katika Baraza la Wawakilishi.
Dk. Mwinyi alimuomba Dk. Magufuli watakapoingia madarakani kuwasaidia katika miradi mikubwa ya kimaendeleo iliyoanzwa na awamu ya saba ikiwemo mradi wa bandari kubwa, barabara, sekta ya maji, umeme na hospitali ya rufaa katika eneo la Binguni ili miradi hiyo iweze kutimia kwa maendeleo ya watu wa Zanzibar.