NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi amesema kipaumbele chake cha kwanza akifanikiwa kushinda urais ni kuhakikisha anakuza uchumi ili wafanyakazi na watumishi waweze kutononoka kimaslahi.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana huko katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil alipokuwa akizungumza na viongozi wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar (ZATUC).

Alisema serikali yake atakayoiunda itakuza uchumi ili iweze kukusanya fedha za kutosha ambazo zitawezesha wafanyakazi kupata stahiki zao yakiwemo maposho na marupurupu mengine.

Dk. Mwinyi alisema serikali ya awamu ya nane itajipambanua kwa ajili ya kukuza uchumi ili iweze kuwahudumia vyema watumishi na wafanyakazi wake na kwamba amefarajika kusikia changamoto zinazowakabili wafanyakazi na kuahidi kuzifanyia kazi.

Mgombea huyo alisema endapo akifanikiwa kushinda katika uchaguzi ujao atahakikisha wafanyakazi wanakuwa na mawasiliano ambayo yatafanikisha kuondosha changamoto zilizopo.

“Nimegundua kuwepo kwa changamoto ya kutokuwepo kwa mawasiliano katika maeneo ya kazi. Changamoto nyengine zilizopo zinaondoka kwa mazungumzo tu na si jambo jengine”, alisema.

Alifahamisha kuwa katika uongozi wake atahakikisha viongozi wanaopewa nafasi ya kusimamia taasisi na idara atahakikisha wanawajibika katika maeneo yao ya utumishi.

Alisema wapo baadhi ya viongozi wanapewa nafasi za uongozi, lakini kwa bahati mbaya baada ya kupata nafasi hizo hawashughulikii wafanyakazi wa chini ikiwemo kushindwa kuzisimamia haki zao.

Hata hivyo, alifahamisha kuwa suala la haki na wajibu katika kazi ni muhimu hivyo, ili serikali iweze kuwapa haki wafanyakazi, lazima watumishi nao wawajibike katika maeneo yao ya kazi.

“Mimi niwaahidi, kuweni na matumaini na mimi, naweka ahadi kwenu na najua ahadi ni deni”, alisema.