MADINA ISSA  NA HAJI  NASSOR,PEMBA 

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar atawahamasisha  wafanyabiashara wote wakubwa Zanzibar kudhamini michezo pamoja na kulitafutia ufumbuzi suala la migogoro ya vyama vya michezo.

Aliyasema hayo, alipokuwa akizungumza na wanamichezo mbalimbali wa visiwa vya Pemba katika ukumbi wa Misali uliopo Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema  kwa kuda mrefu kumejitokeza migogoro mbalimbali katika vyama vya michezo jambo ambalo linaweza kuzoretesha michezo Zanzibar.

Hivyo, ameahidi endapo atachaguliwa atatatua migogoro iliyopo ikiwemo  masuala ya matumizi ya fedha .

Aidha Dk.Mwinyi, alisema atahakikisha ana washirikisha vya kutosha wafanyabiashara hao ili waweze kudhamini ligi kuu zote za Zanzibar na si za mpira wa miguu peke yake.

Pamoja na hayo Dk.Mwinyi alisema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar atahakikisha serikali atakayoiongoza itahakikisha inatenga fungu maalum kwa ajili ya kukuza michezo.

Aidha alisema lazima sekta binafsi zishirikishwe katika maendeleo ya michezo Zanzibar.

“Michezo haiwezi kwenda mbele kama hatujazungumzia fedha  hivyo ni lazima tutafute njia ya kupata fedha ili michezo yetu Zanzibar isonge mbele,” alisema.

Mbali na hayo Dk. Mwinyi alisema, endapo ataingia madarakani atahakikisha kuwa anajenga vyama  imara vya  michezo ambavvyo vitakuza michezo nchini.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alisema kila mmoja akitimiza majukumu yake kwa kuona changamoto zote zinazoikabili sekta ya michezo basi michezo ya Zanzibar itakuwa.

Alisema kwa upande wa serikali kuna majukumu manne makubwa, kwanza ni sera ambapo alisema lazima kuwe na sera nzuri ya michezo.

“Nimeambiwa kama kuna sera mpya ambayo tutaitizama tuone kama inajibu changamoto hizi na kama kuna haja ya kurekebisha basi irekebishwe,” alisema.