Asema wana mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi

Awaahidi kuwatumia watakaorudi nchini

NA KHAMISUU ABDALLAH

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali ya awamu ya nane inakusudia kukuza uchumi kwa kushirikiana na jamii ya Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi ‘Diaspora’ ili kufikia malengo.

Kauli hiyo aliitoa jana, wakati akizungumza na wanajumuiya hiyo katika hoteli ya Park Hayyat, Forodhani ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za kukutana na makundi mbalimbali.

Alisema, ‘diaspora’ wana mchango mkubwa wa kusaidia uchumi wa nchi kwa kuwekeza nchini ili Tanzania ikiwemo Zanzibar katika hatua za kimaendeleo.

Alisema iwapo atapata ridhaa ya kuingia madarakani atahakikisha anaweka mazingira mazuri kwa diaspora ili kuendelea kusaidia maendeleo ya nchi yao.

Dk. Mwinyi, aliwapongeza kwa utayari wao katika kuwasaidia Wazanzibari wenzao ambayo ndio azma ya serikali kushirikisha watu mbalimbali waliopo katika nchi mbalimbali kusaidia nchi yao.

“Azma ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni kuleta mapinduzi ya kiuchumi kupitia umoja wenu tunahitaji sana kupata wataalamu wazalendo ambao mtasaidia kukuza uchumi wetu kupitia dhana ya uchumi wa bahari kuu,” alisema.

Dk. Mwinyi aliwahakikishia Wazanzibari nje ya nchi ambao wapo tayari kurudi nyumbani basi serikali ipo tayari kuwatumia katika utaalamu wao kupitia sekta mbalimbali nchini.

Hata hivyo, alisema anatambua juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya saba kwa kutengeneza sera na sheria ya diaspora na kuahidi atakapoingia madarakani itaaza kutekelezwa mara moja.

Aliwaomba kuendelea kutoa msaada katika nchi yao na kufikiria kufanya makubwa zaidi hasa kuona huduma za kibingwa zinafanyika hapa hapa Zanzibar.

“Tunataka kuwa na spitali ya rufaa ambayo itakuwa na wataalamu mbalimbali hatutaki kuona mgonjwa wa moyo anapelekwa sehemu nyengine lengo letu atibiwe hapa hapa kama wanavyofanya wenzetu Tanzania bara kwa hospitali ya Jakaya Kikwete,” alibainisha.

Alisema katika kufanikisha hilo ni jukumu la serikali kuona inaweka mazingira mazuri ikiwemo vifaa tiba na mambo mengine muhimu.

Sambamba na hayo akizungumzia uchumi wa bluu alisema serikali inataka utalii ambao utanufaisha nchi ikiwemo utalii wa kisasa wa aina zote ili uweze kukuza pato la Taifa.

“Kwa kweli bado hatujautumia uchumi unaotuzunguka sasa imefika wakati kuitumia ili kuona unatunufaisha wazanzibari na mapato yetu yazidi kukuwa,” alisema.

Kwa upande wa gesi na mafuta alisema imefika wakati kwa wazanzibari kutokuwa watazamaji na kuwa tayari kufanya kazi katika sekta hiyo kwani utafiti unaonesha kwamba Zanzibar ina mafuta ya kutosha.

Hata hivyo, alibainisha kwamba ili uchumi uweze kukua basi nchi inahitaji miundombinu ikiwemo bandari, umeme na mambo mengine muhimu ambayo yatafanikisha kufikia katika lengo la serikali ya awamu ya nane.

Nae, Mkurugenzi Idara ya ushirikiano na uratibu wa Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi, Adila Hilal Vuai, alisema lengo la diaspora ni kushirikiana katika maendeleo ya nchi yao ikiwa ni dhamaira ya serikali ya awamu ya saba chini ya Dk. Ali Mohamed Shein.

Alisema, wapo Wazanzibari wanaoishi nchi mbalimbali ikiwemo Denmamk Oman, Uingereza, Japan, Ethiopia, China, Canada ambao wamekuwa wachangiaji wakubwa kupitia sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu na afya.

Nao Wanadiaspora hao, walisema wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kutokubalika kumiliki ardhi kwa kisingizio sio wazawa na kutotambulika na masheha katika maeneo husika.

Walimuomba Dk. Mwinyi kuanzisha wizara ya diaspora itakayowashughulikia ili kuleta mabadiliko ya haraka nchini kwao.

Mohammed Mansour alisema hotuba ya mgombea huyo imetoa mwanga mkubwa katika kubadilisha uchumi wa nchi na wananchi wake kupitia nyanja mbalimbali zilzokuwepo nchini.

Sambamba na hayo alimpongeza Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuanzisha Idara hiyo ambayo inawashughulikia Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi.