NA KHAMISUU ABDALLAH

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi ameahidi kuwa endapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo, atashirikiana na wawekezaji watakaokuwa tayari kuwekeza miradi hapa visiwani.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Unguja, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Abla iliyopo Mtoni.

Alisema lengo la serikali kuvutia wawekezaji ni kuhakikisha wananchi hasa vijana wanapata ajira pamoja na wawekezaji hao kulipa kodi itakayoisaidia serikali kupata mapato ya kufadhili miradi ya maendeleo.

Alisema sekta ya biashara na uwekezaji wa viwanda ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya Zanzibar, kwani viwanda vinasaidia kuinua sekta ya ajira hasa kwa vijana.

Alibainisha kuwa Zanzibar ikifanikiwa kuwa na viwanda vingi ndipo wananchi watakavyoweza kuzalisha malighafi ambazo zitatumika katika viwanda hivyo.

Aliwahakikishia wafanyabiashara hao kuwa serikali ya awamu ya nane itaweka mkakati maalum wa kuanzisha viwanda hivyo na kuona vinafanya kazi kwa maslahi ya taifa kwa ujumla.

“Tunataka tukae chini na wenye viwanda ili tuweze kuvilinda na wao wahakikishe wananunua malighafi inayozalishwa na wananchi wetu kuona nao wanajipatia kipato,” alisema.

Dk. Mwinyi aliahidi kwamba serikali ya awamu ya nane itahakikisha inashirikiana na sekta binafsi katika maendeleo na ajira ili kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unakua.

Akizungumzia lengo la kampeni zake katika kusikiliza kero za wananchi mbalimbali alisema azma yake akiingia madarakani awe anazielewa changamoto zinazowakabili wananchi na kuzifanyia kazi kwa haraka.

“Nimeshasikia na nimeyapokea na ahadi yangu nitafanya kila linalowezekana kuondoa changamoto hizi kwani tunataka maisha ya wazanzibari yawe bora zaidi na kuhakikisha tunaukuza uchumi wa nchi hii” alisema 

Mbali na hayo Dk. Mwinyi aliahidi kusaidia vikundi mbalimbali hasa sekta binafsi kuweza kujiendesha na kufanya maisha yao kuwa bora zaidi.