NA KHAMISUU ABDALLAH
MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi amesema serikali atakayoiongoza itaimarisha mazingira ya walimu wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuongeza posho kwa walimu wakuu na kuwapandisha madaraja.

Alisema walimu ni kundi muhimu katika nchi, hivyo ataimarisha maslahi yao ili waendelee kuzalisha wataalamu watakaotumika katika nchi yao.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na walimu hao katika ukumbi wa makaazi ya wazee Sebleni, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za kukutana na makundi mbalimbali nchini.

Dk. Mwinyi alisema endapo akichaguliwa na kuiongoza Zanzibar, atashughulikia suala la nyongeza za posho na maslahi mengine ya walimu ili walimu watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.

“Sioni tatizo kuongeza posho kwa walimu wakuu, hawa kama serikali itakuwa na uwezo wa fedha kwa mujibu wa taarifa za ZATU (chama cha walimu) inaonesha kuwa ombi hili lilikuwa limekubalika lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu kutokana na ugonjwa wa corona”, alisema.

Kuhusu ombi la kupandisha madaraja walimu kwa mujibu wa sheria ya utumishi, Dk. Mwinyi, alisema jambo hilo ni muhimu kwani humpa heshima mwalimu wa zamani na kumtofautisha na mfanyakazi aliyeajiriwa karibuni.

Akizungumzia ombi la kupatiwa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, alisema ipo haja ya kuhakikisha walimu walioajiriwa wanapewa mikopo ikilinganishwa na ilivyo sasa ambapo wanapewa wasioajiliwa pekee.

“Kwa maoni yangu nitakaowateua katika nafasi zinazohusiana na mambo yenu (walimu) nitahakikisha wanafanya mapitio ya sheria na sera za elimu ili kuleta tija kwenye sekta hii muhimu kwa maendeleo ya nchi na watu wake,” alisema.

Akizungumzia changamoto ya wafanyakazi wa serikali kutopatiwa mikopo na bodi ya mikopo elimu ya juu Zanzibar alisema hoja hiyo haina mantiki kwani wao ndio warudishaji wakubwa wa mikopo hiyo kutokana na tayari wameshaajiriwa.

Dk. Mwinyi alirejea kauli yake kuwa hatokuwa na muhali kwa mtendaji atakaekwenda kinyume na malengo ya serikali atakayoiongoza na kwamba hatokaa kimya bali atachukua hatua kwa kuwa ameamua kuomba urais kuwatumikia wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wenzake Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU), Mussa Omar Tafurwa, alisema walimu wa Zanzibar wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo maslahi yao kutopandishwa madaraja.

Alisema kazi ya ualimu ni kazi ngumu kwa taifa lolote ulimwenguni kwa maendeleo na watu wake kwani huzivaa akili za binadamu jambo ambalo ni hatari.