HABIBA ZARALI NA HAJI NASSOR, PEMBA

NGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amesema iwapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kushika nafasi hiyo, ataimarisha huduma za afya, ili wananchi wapate uhakika wa matibabu.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo jana huko katika uwanjwa wa mpira jimbo la Kiwani wilaya ya Mkoani, kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni wa chama hicho, uliokuwa na lengo la kuwanadi wagombea wa CCM.

Alisema, suala la afya ni miongoni mwa vipaumbele vyake na atapomaliza kuapishwa, suala hilo litakuwa miongoni mwa mambo yatakayopewa umuhimu mkubwa.

Dk. Mwinyi aliahidi kuwa katika kuimarisha huduma hizo, atajenga nyumba za kisasa za madaktari, ili wapate mahala pazuri na salama pakufanyia kazi zao.

Aidha mgombea huyo wa urais aliahidi kuwa, dawa zitapatikana kwa uhakika sambamba na kuajiri kwa wingi madaktari bingwa ili watoe huduma za tiba kwa ufanisi.

Jengine alilowahidi wananchi wa Zanzibar kuwa iwapo atapata ridhaa ni kuimarisha sekta ya elimu, kwa kuwepo maabara za masomo ya sayansi na vifaa vyake.

Katika hatua nyingine mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, alisema anakusudia kuinua uchumi wa wazanzibari, kwa kuanzisha viwanda mbali mbali vikiwemo vya kusarifia mwani.

Hata hivyo alisema mafanikio ya Zanzibar yanategemea sana utendaji kazi wa kila mmoja, hivyo suala la uwajibikaji ni jambo la lazima.

Alisema kuwa, serikali atakayoiongoza hatopenda hata kidogo kuona ndani yake, mna watendaji wasiopenda kuwajibika, kwani wanakuwa kikwazo kufikia maendeleo yaliokusudiwa.

Awali Rais wa Zanzibar wa na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alisema CCM imewaletea kiongozi mchapakazi ambaye atawatumikia wananchi wa Zanzibar.

Alisema sifa za Dk. Mwinyi za nidhamu, uhodari wa kazi, kuwajali watu wote na ubobevu wa uongozi, hanazo mgombea mwengine yeyote kwa nafasi yoyote kutoka vyama upinzani.

‘’Dk. Mwinyi anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais, maana mimi nauwelewa sana na sijaona kiongozi mwengine anaeuweza baada ya mgombea aliyetuliwa na CCM,’’alifafanua.