NA MADINA ISSA

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar,atahakikisha anaendeleza sekta ya michezo ili kuona wanamichezo wanaimarika pamoja na kuikuza sekta hiyo kuwa imara zaidi.

Alisema serikali inawajibu mkubwa kuisaidia sekta hiyo, na atahakikisha anaisaidia kwa kila hali.

Akizungumza katika mahojiano maalum kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), alisema sekta ya michezo sio burudani pekee lakini hivi sasa inawawezesha wanamichezo na wasanii kupata ajira.

Aidha alisema katika serikali ya awamu ya nane itakayoingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu kumalizika atahakikisha anaiangalia sekta ya michezo ili viwango vya michezo vizidi kuimarika zaidi.

Aidha alisema katika uongozi wake atawahamasisha  wafanyabiashara wakubwa wa Zanzibar kudhamini michezo nchini.

Alisema  kumekuwa na migogoro katika vyama vya michezo jambo ambalo linaweza kuzoretesha michezo Zanzibar na kuahidi kutatua migogoro hiyo.

“Nitahakikisha nawashirikisha wafanyabiashara wakubwa kwa kudhamini ligi kuu zote za Zanzibar na sio mpira wa miguu peke yake” alisema.

Pamoja na hayo, Dk.Mwinyi alisema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar atahakikisha serikali atakayoiongoza, itahakikisha inatenga fungu maalum kwa ajili ya kukuza michezo, ili maendeleo ya michezo yaonekane Zanzibar.

Akizungumzia viwanja vya mpira alisema kuwa ataendeleza viwanja vyote vilivyoachwa na serikali ya awamu ya saba, ikiwemo cha Kitogani watakikamilisha ili wananchi waweze kutumia kwa michezo mbalimbali.

“Nafahamu viwanja vipo na vimeimarika chini ya uongozi wa Dk. Shein, nami wananchi mkinipa ridhaa nitahakikisha kuwa viwanja navimalizia” alisema.