NA KHAMISUU ABDALLAH

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo atajenga hospitali ya kisasa katika kijiji cha Uzi na Ng’ambwa, itakayowawezesha wananchi wa maeneo hayo kupata huduma hizo muhimu.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo ikiwa ni muendelezo wa kampeni za kusikiliza kero za wananchi katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Alisema serikali ya awamu ya nane italifanyia kazi suala hilo na kwamba hospitali itakayojengwa itawezesha wananchi wenye matatizo ya kiafya yanayohitaji upasuaji pia kupatiwa haspitalini hapo.

Aliwaeleza wananchi wa vijiji hivyo kwamba, kutokana na jiografia ya kisiwa cha Uzi kuna umuhimu wa kipekee wananchi kupata huduma za afya bila ya kusumbuka kuzifuata kwa masafa marefu.

“Kama kijiji ambacho kinahitaji kusaidiwa basi ni hichi hasa kutokana na mazingira yake yalivyo, mgonjwa hawezi kufika kwa haraka upande wa pili hivyo nitahakikisha hili nalifanyia kazi kwa nguvu zote,” alisema.

Akizungumzia ombi la barabara ya kutoka Unguja Ukuu mpaka Ng’ambwa, aliwahakikishia kusimamia ujenzi wa barabara ya kijiji hicho yenye urefu wa kilomita 3.5 na daraja lake, ambapo itawezesha kuwarahisishia katika huduma zao za kujipatia maendeleo.

Alisema ili kuwa na maendeleo katika eneo ni lazima kuwa na huduma muhimu ikiwemo miundombinu imara ikiwemo daraja na barabara, kwani kutokuwepo kwa mambo hayo huduma nyingi zinaathirika.

Kwa watu wenye ulemavu aliwahakikishia kuendelea kuwasaidia katika kujiendeleza na kuwakomboa kimaisha katika shughuli zao za kujiletea maendeleo kupitia kituo chao kilichokuwepo katika kijiji hicho.

Hata hivyo, alisema ahadi yake kwa wakulima wa mwani atahakikisha anawapatia zana za kisasa na kiwanda maalum cha zao hilo ili kuona zao la mwani linapata soko la uhakika.

Mbali na hayo, alisema lengo la serikali ni kukuza uvuvi katika visiwa vya Unguja na Pemba na kuboresha maisha ya wananchi katika shughuli zao za kujipatia maendeleo.

Dk. Mwinyi, alisema serikali ya awamu ya nane haitakuwa na muhali kwa watendaji ambao hawatokuwa tayari kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.