NA MWANTANGA AME

RAIS Mstaafu wa awamu ya tano, Dk. Salmin Amour Juma, amewataka wananchi wa Zanzibar kutokubali kuchokozeka na wanasiasa wasioitakia mema taifa hili, na badala yake washiriki kuendelea kustawisha amani ya nchi.

Dk. Salmin, aliyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari baada ya kupiga kura katika kituo cha Kilimani Juu, katika skuli ya Jang’ombe msingi Mjini Unguja.

Dk. Salmin, alisema suala la uchaguzi ni jambo la msingi kwani na lenye kupita lakini ndilo linaloamua khatma ya Wazanzibari, na ni vyema wakaona umuhimu wa kudumisha amani, pamoja na kuchagua viongozi wataoweza kuiongoza nchi ili isonge mbele.

Alisema Zanzibar inahitaji kupata viongozi bora watayoipatia nchi maendeleo ambayo wananchi watayatumia ikiwa nchi ina Amani na sio mivurugano kama inayotokea katika mataifa mengine.

Dk. Salmin, aliiombea amani serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na dunia nzima, kwani uchaguzi ni sehemu ya amani ya nchi.

Akizungumzia hali ya uchaguzi, alisema ameridhishwa jinsi wananchi walivyojitokeza kupiga kura huku wakidumisha Amani na aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kuchukua uamuzi ya kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura ili kuchagua viongozi wanaowataka.