Awapongeza kwa kumsaidia majukumu

Asema wamefanikisha utumishi kwa wananchi

NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amewapongeza watendaji wa serikalini kwa kufanikisha vyema utoaji huduma mbalimbali kwa wananchi katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake.

Dk. Shein aliyasema hayo jana katika viwanja vya ikulu mjini Zanzibar wakati akizungumza na vongozi na watendaji wa taasisi za serikali katika hafla ya kuagana na watendaji hao kufuatia miaka 10 ya uongozi wake.

Alisema mafanikio yote hayo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake yalikusudiwa na hayakupatikana kwa bahati mbaya, ambapo yalipangwa vyema na hatimaye kutekelezwa kwa ufanisi.

Dk. Shein alisema ni fahari kubwa kukua kwa uchumi wa Zanzibar hadi kufikia asilimia saba na hatimaye Tanzania ikiwemo Zanzibar kufikia uchumi wa kipato cha kati.

Alisema yote hayo yamefanikiwa kutokana na mipango mizuri iliyowekwa na kasi hiyo iliyotekelezwa na awamu ya saba inatokana na nguvu na ari ya awamu zilizotangulia.

Sambamba na hayo Dk. Shein alibainisha kwamba katika kipindi cha miaka 10 serikali imeweza kutunga sheria 128 kutokana na mahitaji na kwamba zitasaidia sana kusukuma mbele maendeleo ya Zanzibar.

Hata hivyo, alisema sheria mbili alizifanyia uamuzi mgumu ikiwemo sheria ya kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi na sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Alisema, mambo hayo yote ndio utawala bora kwani ni lazima serikali itekeleza majukumu yake kwa uwazi bila ya kutiliwa shaka na dhana pale unapowatumikia wananchi.

“Huwezi kuendesha nchi halafu uwe unaongopa, lazima ueleze wazi mali ulizonazo na umezipata vipi? Lakini uwe muwazi, huu ndio utawala bora naamini watu walisema lakini sina habari kwani nimefanya wajibu wangu”, alisisitiza.

Kwa upande wa sekta ya utalii alisema alipoingia madarakani mwaka 2010 idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii 110,000 hadi watalii laki tano [500,039] mwaka 2019.

Hata hivyo, Dk. Shein alibainisha kwamba anamaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya nchi kutumikia kipindi cha miaka 10 kwa mujibu wa ibara ya 28 kifungu cha 3.

Dk. Shein alibainisha kwamba zipo nchi ambazo hutokea machafuko kutokana na viongozi kukaa kwa muda mrefu madarakani.

Aliwapongeza wale wote aliowaamini na kuwapa uteuzi na kwamba wametekeleza kazi ya kuwatumikia wananchi na kuwasisitiza watendaji wengine lazima wazingatie sheria na kutokiuka kifungu cha katiba ya nchi yao. 

Hata hivyo, alisema katika kipindi cha miaka 51 cha utumishi wake amefanya kazi kwa uadilifu mkubwa katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Sambamba na hayo alibainisha kwamba mara nyingi amekuwa akichota busara za marehemu mzee Abeid Amani Karume kupitia hotuba zake mbalimbali kuanzia miaka ya 60 alizokuwa akizitoa kwa wananchi.

Hata hivyo, alisema yeye na watendaji wote wanawajibika na wanatumika kwa wananchi kwani serikali ni yao na mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe kwa mujibu wa katiba kifungu cha 9.

Katika hatua nyengine Dk. Shein alifungua milango kwa kiongozi yoyote anaetaka busara zake kwenda kwa ajili ya mambo ya maendeleo na sio mambo ya fitna.