Apongeza mafanikio makubwa

Akitaka chuo kiwe ‘Centre of Excellence’

NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amelitaka Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kushirikiana, kuongeza bidii na ubunifu katika kuiendeleza programu ya ufundishaji wa kiswahili ili kufikia dhamira ya kuifanya SUZA kuwa ‘Oxford ya Kiswahili’.

Dk. Shein ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) ametoa rai hiyo jana katika hafla ya kuagwa, baada ya kukiongoza chuo hicho kwa miaka 10, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo Tunguu.

Alisema ni vigumu kuzungumzia historia na maendeleo ya kiswahili bila kuzungumzia utamaduni wa Zanzibar, huku akibainisha kuwa Zanzibar ni nchi ya kiswahili kinachozungumzwa kwa ufasaha katika maeneo ya mjini.

Alisema watu wengi huridhika kupata tafsiri ya maneno kutoka makamusi ya kiingereza kutoka ‘Oxford’ kuliko makamusi mengine duniani, jambo ambalo linaweza kufikiwa nchini kwa kuweka nguvu katika kuikuza na kuiendeleza lugha hiyo.

Aidha, alihimiza umuhimu wa kuimarisha skuli ya kiswahili na lugha za kigeni ili kuifanya Zanzibar kuwa ‘Centre of Excellence’.

Alieleza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imefungua kituo cha kiswahili eneo la Gymkhana hapa Zanzibar, hivyo ni vyema SUZA ikachangamkia jambo hilo na kuwa kituo cha kiswahili.

Alisema jambo la kufurahisha Zanzibar kuwa na Vyuo vikuu vitatu ambavyo kwa wastani hutoa wahitimu 3,000 kila mwaka na kubainisha umuhimu wa wazanzibari kusoma elimu ya juu hapa nchini, kwani itamuwezesha mhitimu kufahamu changamoto ziliopo na jinsi ya kuisaidia jamii.

Akigusia mafanikio ya SUZA katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake, Dk. Shein alisema katika kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa wataalamu, imeanzisha fani mbali mbali ili kwenda sambamba na mahitaji.

Alisema katika kipindi hicho kuna mafanikio makubwa ya kielimu yaliyofikiwa kupitia SUZA, ikiwemo uanzishaji wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba na mafunzo ya Udaktari (Doctor of Medicine), mafunzo yaliyoanza mwaka 2017/2018 na wanafunzi 25 kufaulu na wengine 48 waliofanikiwa kumaliza masomo yao mwaka 2018/2019.