NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping kwa kutimiza miaka 71 tokea kuasisiwa taifa hilo lililopo mashariki ya mbali.

Katika salamu hizo, Dk. Shein alimpongeza rais Xi Jinping kwa kutimiza miaka hiyo tokea kutangazwa rasmi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha Jamhuri ya Watu wa China Hayati Mao Zedong mnamo Oktoba 1, mwaka 1949.

Dk. Shein katika salamu hizo alieleza kuwa kwa niaba ya serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar na wananchi wake wanatoa salamu za pongezi kwa rais Xi Jinping na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa kutimiza miaka 71 tokea kuasisiwa kwa taifa hilo.

Salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wataendeleza umoja na mshikamano walionao kati yao na ndugu zao wa Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya pande mbili hizo.

Aidha, katika salamu hizo Dk. Shein alieleza kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wameridhishwa na mafanikio ya kiuchumi na kijamii yaliyopatikana na Jamhuri ya Watu wa China  katika miaka 71 chini ya uongozi thabiti na wenye mikakati madhubuti wa Chama cha Kikomunisti cha China (CCP).

Dk. Shein aliongeza kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zote kwa pamoja zinajivunia uhusiano na ushirikiano uliopo kati yao na Jamhuri ya Watu wa  China. Hivyo, Dk.Shein alisisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria utaendelea kudumishwa na kuimarishwa kwa manufaa ya pande zote mbili.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo, familia yake pamoja na wananchi wote wa Jamhuri ya Watu wa China afya njema na mafanikio zaidi katika kuuimarisha uchumi wao ambao umekuwa ukiimarika siku hadi siku sambamba na maendeleo yaliyopo.