NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameagana na wasaidizi wake katika ofisi ya faragha na kuwapongeza kwa kushirikiana nae kwa muda wote wa miaka 10 ya uongozi wake.

Dk. Shein aliyasema hayo katika ukumbi wa ikulu jijini Zanzibar wakati akiwapongeza na kuwaaga wafanyakazi wake wa ofisi hiyo sambamba na kula nao chakula cha mchana.

Dk. Shein aliwapongeza wafanyakazi hao kwa kumsaidia katika kutekeleza vyema majukumu yake katika kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wake akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Aliwataka wafanyakazi hao kuendelea kuwa watiifu, waaminifu na wavumilivu hasa ikizingatiwa kwamba ofisi wanayoifanyia kazi ni maalum na muhimu.

Nao wafanyakazi wa ofisi hiyo kwa upande wao walimpongeza Dk. Shein kwa kuwaongoza vyema, kuwalea na kufanya kazi nao vyema.

Aidha walimpongeza kwa kuwavumilia katika kipindi chake chote cha miaka 10 akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Wafanyakazi hao walieleza kuwa wamefarajika kwa kiasi kikubwa na uongozi wake ambao umewafanyia mambo mengi wananchi wote wa Unguja na Pemba.

Walisema uongozi wa Dk. Shein umeacha alama kwenye mambo mbalimbali ya maendeleo ambayo imekuwa kielelezo kizuri cha utumishi wake kwa wananchi.

Sambamba na hayo, wafanyakazi hao walieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika miaka 10 ya uongozi wa Dk. Shein na wao wanaona fahari kwamba mafanikio hayo yamepatikana na wao wakiwa ni sehemu ya wasaidizi wa rais.