Asema amewaachilia tunu ya amani, utulivu

Azindua dira ya kuinuia maisha ya wananchi

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema awamu ya saba ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mambo mengi na kwamba anaondoka kwa kuwaachilia wananchi wa Zanzibar zawadi ya amani na utulivu.

Dk. Shein aliyasema hayo jana katika hafla iliyofanyika viwanja vya Mao Dze Dong, katika hotuba yake ya kuwaaga wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar sambamba na kuzindua dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050.

Alisema mbali ya jitihada alizozichukua za kuwaachia wananchi mifumo na vitu ambavyo vitarahisisha mwenendo wao wa kujipatia huduma za maisha vile vile anawaachia zawadi ya amani na utulivu.

Dk. Shein aliwasishi wananchi kuzidisha upendo, umoja na mshikamano miongoni mwao ili zawadi hiyo anayowaachia iweze kudumu na kung’ara zaidi.

“Zawadi hii ya amani na utulivu mtaweza kuitumia nyinyi na vizazi vitakavyokuja baadae kwa hivyo itunzeni sana na muilinde kwa nguvu zenu nyote”, alisema Dk. Shein.

Alisema kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba bila ya kutetereka kinyume na matarajio ya wale waliokuwa hawaitakii mema imefanya mambo mengi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Alisema serikali imefanikiwa kuyatekeleza mambo ya maendeleo kwa kuzingatia shida na kero kadhaa zilizokuwa zikiwakabili wananchi kwenye huduma za msingi za jamii.

Aliongeza kuwa wananchi wamekuwa wasikivu katika kufuata taratibu na sheria za nchi mambo ambayo taasisi zilizopewa majukumu ya ukusanyaji wa mapato zimeweza kufanya vizuri sana.

Alisema kuwa wananchi wa Zanzibar kila pembe wanathamini jitihada zilizochukuliwa na serikali yao katika kuleta maendeleo yenye manufaa na kuiunga mkono katika shughuli mbalimbali.

Aliwapongeza viongozi wote wakuu wa SMZ na SMT pamoja na uongozi wa wizara ya Fedha na Mipango na wataalamu wote wa Tume ya Mipango kwa kuiwasilisha Dira ya Zanzibar 2015 kwa wananchi pamoja na kuwapongeza wakuu wa vikosi vya SMZ na SMT.