NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein  jana amekwenda hospitali ya Micheweni kuwapa pole wanachama wa CCM waliovamiwa na kupigwa huko katika kijiji cha Kwale, mkoa wa Kaskazini Pemba.

Dk. Shein alifika hospitalini hapo na kupokewa na viongozi mbali mbali wa mkoa na wilaya hiyo na madaktari wa hospitali ya Micheweni wakiongozwa na Daktari dhamana wa hospitali hiyo Dk. Mbwana Shoka Salum.

Akitoa maelezo ya waathirika hao, Daktari huyo alisema wagonjwa hao walipokewa mnamao majira ya saa moja za usiku wakiwa na majeraha makubwa na mmoja kati ya hao Khatib Said Khatib (43) alikuwa katika hali mbaya.

Kwa mujibu wa uongozi wa Jeshi la Polisi viongozi wa mkoa na wilaya walieleza kuwa  tukio hilo limetokea wakati wafuasi wa chama kimoja cha upinzani cha siasa  walipokuwa wakirudi katika mkutano wao wa kampeni huko Chamboni, wilaya ya Micheweni, na kupita katika kijiji cha Kwale na ndipo walipowashambulia kwa kuwapiga wanachama hao wa CCM.

Miongoni mwa waathirika kwenye tukio hilo ni Khamis Hamad Haji (70), Yassir Hemed Abdi (18), Hassan Khamis Hamad (33), Juma khatib Rajab(34), Abdalla Khamis Mbarouk (30), Khatib Said Khatib (43) na Raya Khamis Hamad (24).

Kwa mujibu wa maelezo ya daktari dhamana, alisema kuwa  Khatib Said Khatib (43) ndiye aliyekuwa hali mbaya wakati alipofika hospitalini hapo kutokana na  kuchomwa kisu tumboni na sehemu ya ubavu.

Aliongeza kuwa waathirika wengine walipata majeraha yakiwemo kupigwa na vitu vyenye ncha kali sehemu za kichwani, tumbo na miguu huku Raya Khamis Hamad (24) ambaye ni mjamzito mtoto wa Khatib Said Khatib(43) alipigwa mateke ya tumbo wakati akimuombea baba yake.

Dk. Shein aliwapa pole waathirika hao na kuwaeleza kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko pamoja na wao na itahakikisha inawakamata wahusika wote na baadae kuwachukulia hatua husika za kisheria.

Aliwaeleza wananchi hao kuwa serikali ya Mapainduzi ya Zanzibar itahakikisa inaendelea kuzilinda familia zao, makaazi yao na vipando vyao na mali zao.

Daktari dhamana huyo aliishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuiimarisha hospitali hiyo na kueleza kwua wananchi wa Micheweni wanaridhika na huduma zinazotolewa zikiwemo za upasuaji.

Aliipongeza mashirikiano makubwa yaliyooneshwa na viongozi wa mkoa, wilaya kwa kuwasaida wananchi hao waliopigwa katika muda wote wakiwa hospitalini hapo.

Nae Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohammed Hassan Haji alimueleza Dk. Shein kuwa tayari watuhumiwa 57 wa tukio hilo wameshakamatwa na jeshi lake linaendelea kuwasaka wahusika wengine.

Raya Khamis Hamad akimueleza Dk. Shein maswahibu yaliyomkuta ya kupigwa mateke ya tumbo, ambapo alisema ipo haja kwa vyama vya siasa kuheshimiana kwani si jambo la busara kufanyiana matukio kama hayo.

Nae Khatib Said Khatib alisema imekuwa jambo la kawaida kwa wafuasi wa chama hicho cha upinzani wanapokwenda ama kurudi mikutanoni kufanya vitendo visivyofaa wakati wakipita katika kijiji chao.

Alisisitiza kwamba ipo haja kuzidishiwa ulinzi katika eneo lao kwani mbali ya kipigo alichokipata yeye na wenziwe pia, mazao yake yote yamekatwa huko shambani kwake.

Aliongeza kuwa ni kawaida kwa wafuasi hao wa chama hicho cha upinzani wanapokwenda katika mikutano yao huchukua silaha za jadi ndani ya gari zao.