NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kufanya kazi kwa ari na bidii katika utendaji.

Dk. Shein alieleza hayo katika uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, lililopo Chake Chake, hafla iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa nyumba za Ikulu huko Micheweni.

Aliwataka wafanyakazi wa Ofisi hiyo kuendelea kulinda hadhi na heshima ya ofisi, kuendelea kushirikiana na kuwasisitiza kuwa serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kazi.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Ofisi ya Rais na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ukiongozwa na waziri Issa Haji Gavu kwa kusimamia vizuri kazi za ujenzi wa jengo hilo.

Alisema nyumba za eneo la ikulu zilikuwa zimechakaa sana ndipo, uamuzi wa kuzifanyia matengenezo ulipofanyika na nyengine kujengwa  upya, ambapo kwa upande wa Pemba Ofisi hiyo imefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha Ikulu ya Mkoani na kujenga Ikulu ya Micheweni.

Alisisitiza kwamba majengo yote hayo yamejengwa kwa fedha za serikali na kutaka kutunzwa kwa jengo hilo ili liweze kutumika kwa muda mrefu na kuwataka wafanyakazi waharakishe kuhamia.

Dk. Shein alisisitiza haja ya kuyatunza na kuyalinda mazingira na kueleza kwamba kila mmoja ana jukumu la kulitunza na kulienzi jengo hilo na majengo yote ya Ikulu.

Alieleza azma ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Wakala wa Nyumba na Majenzi, Shirika la Nyumba na Kampuni ya Majenzi ya Serikali ni kusaidia kupunguza gharama za ujenzi kwa majengo ya serikali.

Alisema kuwa uzoefu wa serikali kujenga majengo yake wenyewe unatokana na uzoefu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar mzee mzee Abeid Amani Karume ambapo katika uongozi wake majengo mengi yalijengwa.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa maelekezo na miongozo katika kuhakikisha ujenzi huo unafanyika vyema.

Waziri huyo alitoa shukurani kwa mashirikiano makubwa yaliyofanyika katika ujenzi huo na kumpongeza Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi kwa mashirikiano yake pamoja na maofisa Wadhamini wote walioshiriki.

Mapema katibu mkuu wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Salum Maulid Salum alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa kutia shime ya kulijenga jengo hilo.

Aidha, maamuzi ya ujenzi wa jengo hilo yanaenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya mwaka 2015-2020.

Aliongeza kuwa matayarisho ya ujenzi wa jengo hilo yalianza mwezi Novemba 2018 ambapo Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) walilikagua eneo hilo kimazingira ili kuhakikisha hawaharibu mandhari ya eneo hilo ambalo asili yake lipo karibu na ufukwe wa bahari.