Ahimiza wakongwe kuandika vitabu kunufaisha jamii

Ataka utulivu vyama vya michezo, akemea soka kupelekwa mahakamani

NA ABOUD MAHMOUD

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein amewashauri wanamichezo nchini kuandika vitabu ili kusaidia ukuaji wa sekta.

Dk. Shein aliyasema hayo jana wakati akizindua kitabu cha ‘mwalimu bora wa soka’ kilichoandikwa na mwanamichezo Ghulam Abdullah Rashid katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni mjini Unguja.

Alisema hastua hiyo itasaidia kuweka kumbukumbu kwa kuwa zanzibar ina hazina ya wanamichezo ambao itawasaidia vijana wa baadae e kujifunza na kufikia malengo yao katika fani hiyo.

“Natoa ushauri kwa wanamichezo kutunga vitabu vitakavyokuwa na maudhui ya michezo hususan soka na vizuri zaidi viandikwe na wanasoka wakongwe kuelezea historia ya mchezo huo hapa visiwani kwetu,” alisema.

Dk. Shein alisema sifa ya mwandishi mzuri ni yule mwenye kufuata nidhamu ya hali ya juu na kuyakumbuka yale yaliofanyika nyuma ambayo yana manufaa kwa taifa.

Alieleza kwamba mtunzi wa kitabu cha mwalimu bora wa soka hakuandika kwa kubahatisha bali aliandika kwa weledi mkubwa unaotakiwa.

Hivyo Dk. Shein alitoa wito kwa viongozi na wachezaji wa soka sasa kujipanga kujipanga kwa nidhamu nzuri ambayo itawasaidia kusifika na kuwatangaza vizuri.

“Ndugu zangu wanamichezo na wapenda michezo kwa ujumla mnunue kitabu hichi ili muweze kujifunza mambo mbali mbali yanayohusiana na soka na ambayo yanakusaidieni katika kuleta maendeleo katika kazi yenu hiyo,” alieleza.